Kwa nini Rais Mnangagwa wa Zimbabwe anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu?
Mgawanyiko unaendelea kushuhudiwa ndani wa chama tawala cha ZANU-PF nchini Zimbabwe umeibua hofu ya uwezekano wa jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Mnangagwa, ambaye anajaribu kusalia madarakani baada ya mwaka 2028 licha ya kuwa ni kinyume na katiba.
Mgawanyiko wa ndani katika chama tawala cha ZANU-PF, ambacho kimekuwa madarakani tangu Zimbabwe ipate uhuru mwaka 1980, ndio chanzo cha mgogoro wa sasa.
Pande mbili kuu zinazozana, moja inamuunga mkono Mnangagwa ambaye ana umri wa miaka 82 aendelee kusalia madarakani, na upande wa pili unamuunga mkono Constantino Chiwenga, makamu wake wa Rais mwenye umri wa miaka 68.
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa anakabiliwa na kile kilichotajwa na weledi wa masuala ya kisiasa kuwa ni tishio kubwa zaidi kwa utawala wake huku vita vya kuwania madaraka vikiibuka kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika 2028.
Hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na Rais na wale wote wanaomuunga mkono kwa lengo la kurefusha muda wa kusalia madarakani hadi mwaka 2030 zimekabiliwa na upinzani na malalamiko ya upande wa pili kutoka ndani ya chama chake mwenye wakimtaka ajiuzulu.
HItilafu hizi tajwa ndani ya chama tawala cha ZANU-PF zimepelekea kufutwa kazi maafisa usalama wa ngazi ya juu; hatua ambayo imetajwa na weledi wa mambo kuwa imechukuliwa na Rais Mnangagwa ili kuepuka kuondolewa madarakani kupitia mapinduzi.
Zimbabwe kwa miongo kadhaa sasa imezama katika migogoro ya kisiasa ambayo imesababisha kudorora kwa uchumi, uhaba wa ajira n.k.
" Wazimbabwe wamechoka na wanahitaji mkombozi,” amesema Blessing Vava, Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea haki za binadamu la Crisis Zimbabwe.