Dec 04, 2023 03:39 UTC
  • Mafuriko na maporomoko yaua watu 47, yajeruhi 85 mkoani Manyara Tanzania

Mkuu wa Mkoa wa Manyara ulioko kaskazini mwa Tanzania amesema, hadi kufikia jioni ya jana watu 47 walikuwa wamefariki dunia na wengine 85 kujeruhiwa wilayani Hanang mkoani humo kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jana.

Mvua hiyo ilisababisha sehemu ya Mlima Hanang kumomonyoka na kusababisha kutiririka tope katika maeneo ya Katesh na Gendabi.

Queen Sendiga amesema, watu wengine wanahofiwa kufukiwa na tope baada ya nyumba na makazi yao kusombwa na mafuriko ya maporomoko ya udongo huo kutoka Mlima Hanang.

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, mkuu wa mkoa wa Manyara amesema, eneo kubwa lililoathiriwa na mafuriko hayo ni Kata ya Gendabi na katikati ya Mji wa Katesh, ambayo ni makao makuu ya wilaya ya Hanang mkoani humo.

"Nyumba za watu zimezingirwa na mafuriko na miti iliyosombwa; na mafuriko kutoka sehemu ya mlima Hanang yamesababisha barabara ya Katesh kwenda Singida kushindwa kupitika," amesema Sendiga.

Rais Samia Suluhu Hassan

Mapema jana, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ambaye yuko Dubai, Muungano wa Falme za Kiarabu anakoshiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) alitoa mkono wa pole na salamu za rambirambi kwa wananchi na waathirika wa mafuriko hayo na kuagiza nguvu zote za Serikali zielekezwe katika eneo hilo kwa ajili ya uokozi na kuzuia maafa zaidi.

"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa kuhusu mvua kubwa iliyonyesha mkoani Manyara na kuleta madhara makubwa Katesh. Tunatoa pole kwa waathirika wa tukio hilo", ameeleza Rais Samia na kuongezea kwa kusema: "nimeelekeza nguvu zote za Serikali zielekezwe katika uokozi ili kuzuia maafa mengi...tumesikitishwa na tukio hili, lakini ndio mipango ya Mungu inavyokwenda".../

 

Tags