Wawakilishi wa Hamas washiriki katika kumbukumbu ya kumuenzi Mandela
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i105672-wawakilishi_wa_hamas_washiriki_katika_kumbukumbu_ya_kumuenzi_mandela
Maafisa wakuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) jana Jumanne waliungana na familia ya Nelson Mandela katika kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo cha rais huyo wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, mjini Pretoria.
(last modified 2023-12-06T09:23:37+00:00 )
Dec 06, 2023 09:23 UTC
  • Wawakilishi wa Hamas washiriki katika kumbukumbu ya kumuenzi Mandela

Maafisa wakuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) jana Jumanne waliungana na familia ya Nelson Mandela katika kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo cha rais huyo wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, mjini Pretoria.

Shujaa wa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, Mzee Nelson Mandela, ambaye alitetea "uhuru wa Wapalestina", alifariki dunia mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 95. Viongozi kutoka sehemu mbalimbali za dunia, akiwemo Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas, walihudhuria mazishi yake, lakini viongozi wa Israel hawakuhudhuria.

Basem Naim, waziri wa zamani wa afya wa Hamas huko Gaza, na Khaled Qaddoumi, mwakilishi wa harakati hiyo nchini Iran, wameshiriki katika kumbukumbu ya Mzee Mandela mjini Pretoria. Mapema viongozi hao wa Hamas, pia walikuwa wameshiriki katika mkutano uliojadili mgogoro wa Israel na Palestina ulioandaliwa na mjukuu wa Nelson Mandela, Mandla Mandela, mjini Johannesburg.

Akihutubia watu walioshiriki shughuli ya kumuenzi Mandela, mjukuu wake, Mandla Mandela amesema: "Tulitaka kujionea na kusikia moja kwa moja ukatili unaofanywa kila siku huko Gaza." 

Zwelivelile Mandla Mandela

"Ilikuwa uzoefu halisi kwao kuwa Afrika Kusini na kujifunza kutokana na yale tuliyopitia wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi, mojawapo ya tawala za kikatili zaidi katika bara la Afrika, ambao tuliushinda", amesema Mandla Mandela na kuongeza kuwa, anataka kuendeleza kazi ya babu yake kwa ajili ya kuundwa taifa huru la Palestina. 

Chama tawala nchini Afrika Kusini, African National Congress (ANC), mwezi uliopita kiliunga mkono hoja katika Bunge la Taifa ya kutaka kufungwa ubalozi wa Israel na kusitishwa uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo. Chama hicho pia kinapinga vikali mashambulizi ya kikatili yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza. 

Pretoria pia imeitaka rasmi Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuchunguza "uhalifu wa kivita" uliofanywa na Israel huko Gaza.