Dec 13, 2023 11:16 UTC
  • Niger: Askari wote wa Ufaransa wawe wameondoka nchini ndani ya siku 10

Jeshi la Niger limetangaza kuwa, askari wote wa Ufaransa walioko nchini humo watakuwa wameondoka kikamilifu katika ardhi ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufikia Disemba 22.

Taarifa ya baraza la kijeshi linalotawala Niger imesema: Mpaka sasa, wanajeshi 1,346 wa Ufaransa pamoja na asilimia 80 ya zana zao za kilojistiki wameondoka nchini. 

Jeshi la Niger limebainisha kuwa, kufikia sasa ni wanajeshi 157 pekee kati ya askari wote 1,500 wa Kifaransa ndio wamesalia nchini humo, na wanatazamiwa kuondoka nchini humo kufikia Disemba 22.    

Ufaransa ilianza zoezi la kuwaondoa wanajeshi wake nchini Niger mwezi Oktoba mwaka huu, baada ya kutimuliwa na baraza la kijeshi linalotawala nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Waniger wamekuwa wakiandamana wakitaka askari vamizi wa Ufaransa waondoke nchini humo

Jumamosi iliyopita, watu wa matabaka mbalimbali, taasisi na mashirika ya kisiasa na ya kiraia ya Niger walishiriki kwa wingi katika maandamano dhidi ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS na waungaji mkono wa siasa za ubeberu wa Ufaransa.

Waandamanaji hao mjini Niamey walipiga nara dhidi ya siasa za ubeberu za Ufaransa na ECOWAS na kupeperusha bendera za Niger, Burkina Faso na Mali na kusisitiza juu ya suala la kujitawala na kuwa huru nchi yao.

Uhusiano wa Niger na Ufaransa uliharibika zaidi Julai mwaka huu, baada ya jeshi kumpindua rais ambaye wananchi wa Niger walikuwa wanalalamika vikali kwamba ni kibaraka mkubwa wa Ufaransa, Mohammad Bazoum.

Tags