Misri: Mazungumzo na Bwawa la Renaissance yamefeli
(last modified Wed, 20 Dec 2023 06:20:40 GMT )
Dec 20, 2023 06:20 UTC
  • Misri: Mazungumzo na Bwawa la Renaissance yamefeli

Misri imetangaza kwamba mazungumzo kuhusu Bwawa la Renaissance nchini Ethiopia yamemalizika bila mafanikio, na imeishutumu Addis Ababa kuwa imekataa masuluhisho yote yaliyopendekezwa kwa ajili ya kutatua mzozo wa ujenzi wa bwawa bilo juu ya maji ya Mto Nile.

Cairo imesisitiza kuwa inahifadhi haki ya kulinda usalama wake wa maji.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Kilimo cha Umwagiliaji ya Misri imesema kwamba, mkutano wa nne na wa mwisho wa mazungumzo na nchi za Ethiopia na Sudan kuhusu Bwawa la Renaissance ulimalizika jana bila kupatikana matokeo yoyote, na kuongeza kuwa Misri itafuatilia kwa karibu mchakato wa kujaza maji na kuendesha bwawa hilo.

Wizara hiyo imeongeza kuwa kwa kuzingatia misimamo hiyo ya Ethiopia, "njia ya mazungumzo imefikia ukingoni" na kwamba kwa mujibu wa mikataba na makubaliano ya kimataifa, Misri inahifadhi haki yake ya kutetea usalama wake wa maji na wa taifa endapo itakabiliwa na madhara.

Hakujatolewa taarifa yoyote kutoka Upande wa Ethiopia au Sudan kuhusu mazungumzo hayo yanayoyumba ambayo yalianza takriban muongo mmoja uliopita kuhusu ujenzi wa Bwawa la Renaissance juu ya maji ya Mto Nile.

Misri na Sudan zinahofia bwawa hilo kubwa lililoghrimu dola bilioni 4.2 litapunguza kwa kiasi kikubwa sehemu ya maji ya Mto Nile wanayopokea, na mara kadhaa zimeiomba Addis Ababa isitishe kulijaza hadi makubaliano yafikiwe.