Dec 21, 2023 11:23 UTC
  • WFP yasimamisha usambazaji wa chakula Sudan, mapigano yaenea

Mpango wa Chakula Dunia (WFP) umesimamisha kwa muda utoaji na usambazaji wa chakula katika baadhi ya maeneo katika jimbo la al-Jazira katikati ya Sudan, huku mapigano yakipanuka na kuenea pande za mashariki na kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum.

Eddie Rowe, Mwakilishi na Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, timu za shirika hilo la Umoja wa Mataifa zinafanya hima kuendelea kusambaza chakula cha msaada katika maeneo ambayo yangali na utulivu.

Taarifa ya WFP imeeleza kuwa, watu zaidi ya laki tatu (300,000) wamekimbia makazi yao ndani ya siku chache zilizopita katika jimbo la al-Jazira kutokana na kushtadi mapigano ambayo yaliripuka katika eneo hilo Ijumaa iliyopita.

Taarifa ya WFP imekuja siku chache baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa, Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinapigana na Jeshi la Sudan nje ya mji wa Wad Madani katika Jimbo la Al-Jazira (katikati ya Sudan), na kwamba mapigano hayo yamelazimisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao na kuelekea katika maeneo salama.

Mji huo ulikuwa umepokea mamilioni ya watu walioukimbia mji mkuu Khartoum, baada ya kuibuka mapigano nchini humo mwezi Aprili mwaka huu. Watu zaidi ya 12,000 wameuawa katika mapigano baina ya pande mbili hizo, wengine 33,000 wamejeruhiwa huku wengine zaidi ya milioni 7 wakilazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.

Mapigano yachachamaa Sudan

Mapema wiki hii, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alitoa mwito kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na Jeshi la Sudan kusitisha uhasama na mapigano mara moja, na kuketi kwenye meza ya mazungumzo kwa shabaha ya kurejesha utulivu, uthabiti na amani endelevu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Moussa Faki Mahamat amesisitiza kuwa, AU ipo tayari kusimamia mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mzozo baina ya pande mbili hasimu za Sudan na kwamba Umoja wa Afrika unatiwa wasi wasi na taarifa za kupanuka mgogoro nchini humo.

 

Tags