Maelfu washiriki kwenye maandamano ya Morocco ya kuunga mkono Palestina
Maelfu ya watu nchini Morocco wamefanya mojawapo ya maandamano makubwa zaidi ya kuunga mkono Palestina mjini Rabat, tangu kuzuka kwa vita vya Gaza, wakati wakiitisha kuvunjwa kwa mahusiano kati ya taifa lao na Israel.
Maandamano dhidi ya vita vya Israel huko Gaza yamekuwa yakivutia maelfu ya watu nchini Morocco, tangu kuanza kwa vita na hujuma za kinyama za Israel zaidi ya miezi miwili iliyopita, mengi yakiongozwa na makundi ya Kiarabu na Kiislamu.
Maandamano ya jana Jumapili yalifanyika kwa ushirikiano na makundi mbalimbali ya kiraia . Wengi wa waandamanaji hao takriban 10,000 walikuwa Waislamu, ambapo wanaume walikuwa kando na wanawake, wakati wakipeperusha bendera ya Palestina, huku baadhi wakibeba mabango na maberamu yenye maneno, “upinzani kuelekea kwenye ushindi,” “ sitisheni uhusiano wa serikali ya Morocco na Israel” pamoja na “ achia Palestina uhuru wake.”

Wananchi wa Morocco hadi sasa wameshaandamana na kumiminika mabarabarani mara kadhaa sambamba na kuzichoma moto bendera za utawala haramu wa Kizayuni, kuonyesha upinzani wao dhidi ya hatua ya serikali ya Rabat kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv na kutaka uhusiano huo ukomeshwe.
Desemba 2020, Morocco na utawala haramu wa Israel zilifikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kwa ushawishi wa Marekani. Na kama sehemu ya makubaliano hayo, Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alikubali kutambua mamlaka ya Morocco juu ya Sahara Magharibi. Hata hivyo serikali ya rais wa sasa wa nchi hiyo Joe Biden imesema itauangalia upya uamuzi huo.