Mvua, maporomoko ya udongo yaua makumi ya watu DRC
Watu wasiopungua 22 wamefariki dunia kutokana na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika mji wa Kananga, katikati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Taarifa ya Ofisi ya Gavana wa Mkoa wa Kasai imesema, miongoni mwa watu walioaga dunia kwenye majanga hayo ya kimaumbile ni mama na wanawe wanane waliokuwa katika nyumba moja, na baba na wanawe wanne katika nyumba nyingine.
Jumapili iliyopita, watu 20 walifariki dunia baada ya kusombwa na maji ya mto uliovunja kingo zake katika mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa DRC.
Aidha haya yanajiri wiki mbili baada ya watu wengine 15 kupoteza maisha katika maporomoko ya udongo katika mji wa Bukavu, makao makuu ya jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mbali na mamia ya watu kuaga dunia, wengine zaidi ya milioni 3 wameathiriwa na mafuriko katika nchi za kanda ya Afrika Mashariki na Kati, ambapo milioni 1.2 kati yao wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na athari za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Hivi karibuni, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilitahadharisha kuhusu tishio linaloongezeka kwa usalama wa chakula katika eneo la Pembe ya Afrika na kanda ya Afrika Mashariki kwa ujumla, kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi za ukanda huo.