Mjukuu wa Mandela: Tutaishtaki Israel katika duru nyingine za kisheria
(last modified Tue, 30 Jan 2024 02:43:35 GMT )
Jan 30, 2024 02:43 UTC
  • Mjukuu wa Mandela: Tutaishtaki Israel katika duru nyingine za kisheria

Mjukuu wa Nelson Mandela, shujaa na kiongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, amesema kuwa nchi yake itawasilisha mashtaka mengine dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika duru nyingine za kisheria, kama Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo.

Hatua hii inafuatia kesi iliyofunguliwa na Afrika Kusini mwishoni mwa mwezi Disemba, katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya utawala wa Israel kwa mauaji ya kimbari ya watu wa Palestina.

Tarehe 29 Disemba Afrika Kusini iliwasilisha mashtaka yake dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki  kwa hoja kuwa utawala huo wa Kizayuni umekiuka Makubaliano ya Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1948 katika mashambulizi yake Ukanda wa Ghaza.

Katika hukumu yake ya awali iliyotolewa Ijumaa tarehe 26 Januari, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) iliuamuru utawala wa Kizayuni wa Israel kuchukua hatua zote zinazohitajika kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari huko Gaza.

Akizungumzia suala hilo, mjukuu wa Nelson Mandela, Zwelivelile "Mandla" Mandela, mapema jana amesema kwamba: Timu ya wanasheria wa Afrika Kusini itafuatilia kesi iliyowasilisha katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki na kwa sasa inasubiri ripoti ambayo Israel itawasilisha ndani ya mwezi ujao ili iweze kuangalia machaguo yaliyopo kwa ajili ya utawala wa Kizayuni na kisha itawasilisha mashtaka dhidi ya Tel Aviv katika duru nyinginezo kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Baraza la Usalama na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Zwelivelile Mandela

Zwelivelile Mandela ameongeza kuwa, vita vya Gaza ni mfano wa wazi wa ubeberu na unafiki wa Kimagharibi, na nchi za Magharibi hazijaweka vikwazo dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel, wala hazijatoa waranti ya kukamatwa waziri mkuu na mawaziri watendajinai wa utawala wa Kizayuni. 

Mjukuu huyo wa Mandela pia ameashiria uhusiano mkubwa na wa kihistoria wa Mandela na kadhia ya Palestina na kusema: "Uhuru wetu haujakamilika bila uhuru wa watu wa Palestina."

Zwelivelile Mandela amesema kwamba dhamira yao ya kutetea Palestina ilianza katika siku za giza za kupigania uhuru wa Afrika Kusini, na kuongeza kuwa: "Babu yangu, Nelson Mandela, alisema kuwa alipohukumiwa kifungo cha maisha katika kisiwa cha Robben, alipata msukumo wa kuendelea kupigania uhuru kutokana na mapambano ya kupigania uhuru ya Wapalestina.