Feb 17, 2024 12:25 UTC
  • Mashirika yaitaka AU isiipe Israel uanachama kwenye umoja huo

Kundi moja la asasi za kiraia limeutaka Umoja wa Afrika utupilie mbali ombi la utawala wa Kizayuni wa Israel la kuwa mwanachama mtazamaji wa AU, na kufufua mjadala uliodumu kwa miaka miwili kuhusu kadhia hiyo.

Taasisi na shakhsia 151 kutokana bara Afrika, wawakilishi wa Waafrika walioko ughaibuni, wameitaka AU isikubali kuburuzwa kuipa Israel uanachama katika umoja huo.

Mashirika hayo yasiyo ya kiserikali yamesema kuinyima Israel uanachama katika Umoja wa Mataifa kutatuma ujumbe wa wazi kwa walimwegu kuwa jinai zinaweza kuadhibiwa hata na mnyonge.

Kundi hilo la kiraia linalojiita 'Pan-African' limemuandikia barua Mwenyekiti anayeondoka wa AU, Azali Assoumani (Rais wa Comoro) likimtaka asimame kidete na kuwatetea wananchi wanaokandamizwa wa Palestina.

Huku Mkutano wa 37 wa Kawaida wa Viongozi wa Umoja wa Afrika ukianza Addis Ababa, Ethiopia leo, asasi hizo za kiraia zimesema zinapinga vikali kupewa uanachama utawala wa Kizayuni katika AU, na kuutaka umoja huo ulinde hadhi na thamani ya asasi hiyo kuu ya bara la Afrika.

Taasisi hizo zimeishutumu Israel kwa kukataa kuheshimu Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari wa mwaka 1948, huku zikitaka jamii ya kimataifa zichukue hatua za kukomesha umwagaji damu unaofanywa na Israel huko Gaza.

Mashariki hayo pia yamepongeza uamuzi wa Umoja wa Afrika wa kusimamisha hadhi ya uanachama mtazamaji wa utawala wa Kizayuni katika jumuiya hiyo ya kibara.

Itakumbukwa kuwa, Mkutano wa 35 wa wakuu wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Februari 2022 huko Addis Ababa, Ethiopia ulisitisha hadhi ya utawala ghasibu wa Israel ya kuwa mwanachama mtazamaji katika umoja huo.

Tags