Apr 20, 2024 07:46 UTC
  • Faure Gnassingbe
    Faure Gnassingbe

Bunge la Togo jana Ijumaa liliidhinisha mageuzi ya Katiba ambayo yanabadili mfumo wa utawala wa nchi hiyo kuelekea kwenye utawala wa Bunge. Mabadiliko hayo yamekosolewa na vyama vya upinzani vinavyosema kuwa yanamruhusu Rais Faure Gnassingbe kuendelea kung'ang'ania madaraka.

Hatua hiyo imekuja siku chache kabla ya uchaguzi wa Bunge wa Aprili 29 nchini Togo, ambapo upinzani umepuuzilia mbali mageuzi hayo na kusema ni "mapinduzi ya kikatiba" ya kuunda wadhifa mpya wa uwaziri mkuu ambao wapinzani wanasema utamruhusu rais wa Togo kuepuka ukomo wa mihula ya kusalia madarakani.

Bunge la Togo lilikuwa tayari limepitisha katiba mpya mnamo Machi 25, lakini Rais Gnassingbe aliwaomba wabunge kupiga kura tena baada ya mageuzi hayo kuzua mvutano wa kisiasa.

Vyama vya upinzani vinayaona marekebisho hayo kama njia ya kumuongezea muda Gnassingbe, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2005 baada ya kumrithi babake ambaye mwenyewe alitawala taifa hilo dogo la Afrika Magharibi kwa takriban miongo minne.

Katiba ya sasa ingemruhusu kiongozi huyo wa Togo kugombea muhula mmoja wa mwisho mwaka wa 2025.