May 04, 2024 09:53 UTC
  • Wanajeshi DRC wahukumiwa kifo kwa kosa la kukimbia vita

Mahakama ya kijeshi katika mji wa Goma huko Kivu Kaskazini ashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewahukumu kifo maafisa wanane wa jeshi la Congo, FARDC kwa tuhuma za kukimbia vita na kutoheshimu sheria za kijeshi. Miongoni mwao ni Kanali Shamba mkuu wa kikosi cha makomandoo pamoja na msaidizi wake.

Mwendesha mashtaka amesema makamanda hao walishindwa kuwajibika kwenye uwanja wa mapambano karibu na mji wa Sake wilayani Masisi eneo lililo magharibi mwa mji wa Goma ambako M23 wanaendelea kuchukua udhibiti wa vijiji.

Wakili wa makamanda hao Bwito Jean Richard wa jeshi tiifu kwa serikali amesema kuwa, mahakama imefanya makosa kutoa adhabu ya kifo kwa wanajeshi hao ambao walikuwa wamejitolea kulipigania taifa.

Wakili huyo amekata rufaa na kuionya Mahakama kuwa makini kwa kuwa hatua za mahakama zinaweza kuwapelekea wanajeshi wengi kutokwenda vitani.

Wakati wa kusikilizwa kesi ya wanajeshi wa DRC wanaokabiliwa na tuhuma za kukimbia vitani

 

Pamoja na hayo baadhi ya wachambuzi wanasema, hatua hii itawazuia wanajeshi kukimbia mapigano kila mara na kuwaacha waasi kuchukua vijiji.

Katika hukumu hiyo wanajeshi watatu, kapteni mmoja na maluteni wawili waliachiliwa huru na mahakama baada ya mahhakama kusema kuwa, hhawana hatia.

Makamanda hao walipewa adhabu ya kifo kwa mujibu wa sheria ya nchi hiyo. Wakati huohuo Mkuu wa mahakama ameziomba pande husika kukata rufaa katika kipindi cha siku tano.