May 04, 2024 09:53 UTC
  • Uingereza sasa kuwapeleka nchini Rwanda waomba hifadhi

Serikali ya Uingereza imeiambia Mahakama Kuu mjini London kwamba inatarajia safari za kwanza za ndege za kuwapeleka wahamiaji kwenda Rwanda zitaanza kati ya Julai Mosi na Julai 15 mwaka huu.

Jaji Martin Chamberlain alifichua tarehe hizo wakati alipokuwa akipanga kusikilizwa kwa pingamizi lijalo la kisheria kwa sera tatanishi ya taifa hilo kutoka kwa chama cha wafanyakazi wa umma-FDA.

Aprili 22, Waziri Mkuu Rishi Sunak alisema kwamba alitarajia safari za kwanza za ndege kuondoka ndani ya "wiki 10 hadi 12", lakini hakutoa tarehe kamili.

Serikali ya Uingereza imeeleza kuwa timu za utendaji ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani zimekuwa zikifanya kazi kwa kasi kuwaweka kizuizini kwa usalama na haraka watu walioorodheshwa katika mkakati huo wa Waziri Mkuu Sunak ili kupatiwa hifadhi huko Rwanda.

Mawaziri wa Rwanda na Uingereza wakitiliana saini makubaliano ya kuwapeleka Rwanda wahamiaji wanaoomba hifadhi nchini Uingereza

 

Ripoti kutoka taasisi ya kujitolea ya kuhudumia wakimbizi ya Care4Calais imethibitisha kuwa zoezi la kuwakamata na kuwashikilia raia hao wanaotazamiwa kupelekwa Rwanda lilianza Jumatatu iliyopita.

Mahakama ya Juu ya Uingereza ilisema mwaka uliopita kwamba, mpango wa serikali ya London wa kuwapeleka nchini Rwanda wakimbizi na waomba hifadhi walioko nchini humo unakiuka sheria. Ilisema mpango huo unawaweka katika hali hatarishi wakimbizi hao, hasa kwa kuzingatia kuwa baadhi yao waliikimbia nchi yao ya Rwanda, na kuwarejesha huko ni kutawaweka hatarini. 

Kwa mujibu wa Kamishna wa Haki za Kibinadamu wa Baraza la Ulaya, Michael O'Flaherty, mpango huo wa serikali ya Kigali na Uingereza, unaibua maswali mengi kuhusu haki za waomba hifadhi na sheria kwa ujumla.