Kushindwa kijiopolitiki Marekani barani Afrika
Kama ilivyotarajiwa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imelazimika kukubali kuwaondoa huko Niger wanajeshi wote elfu moja wa nchi hiyo.
Marekani ilitangaza mwezi Aprili kuwa inaanza kuratibu mpango wa kuwaondoa taratibu wanajeshi wake huko Niger hata hivyo viongozi wa Marekani wanaendelea kufanya mazungumzo na watawala wa kijeshi wa Niger ili kuwabakisha katika nchi hiyo ya Kiafrika baadhi ya wanajeshi wake.
Afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka kutaka jina lake ameliambia jarida la Politico kuwa matumaini ya kubakia baadhi ya wanajeshi wao wiki iliyopita huko Niger yametoweka na kwamba Pentagon imeagiza kuondolewa wanajeshi wake wote elfu moja katika nchi hiyo. Afisa huyo ameongeza kuwa muda wa kuondoka wanajeshi hao unaweza kubadilika na kuwa watahamishiwa katika kambi nyingine katika eneo hilo.
Niger hadi sasa imekuwa na nafasi muhimu katika oparesheni za kijeshi za Marekani katika eneo la Sahel Afrika na ni mwenyeji wa kambi kubwa ya anga ya Marekani. Serikali ya Marekani inasema kuwa imetumia mamia ya mamilioni ya dola kutoa mafunzo kwa vikosi vya jeshi la Niger.
Baada ya mapinduzi ya Niger, watawala wapya wa nchi hiyo walichukua hatua haraka ya kuvunja uhusiano wa kijeshi na nchi za Magharibi na hasa Ufaransa na Marekani; na kujikurubisha zaidi kwa nchi kama China na Russia. Hii ni katika hali ambayo Baraza la kijeshi linaloongoza huko Niger limetangaza kuwa kuwepo kijeshi Marekani nchini humo ni kinyume cha sheria na kukosoa oparesheni za Pentagon nchini humo. Weledi wa mambo wameashiria kufikia ukomo uwepo kijeshi wa Marekani huko Niger na kuwasili nchini humo wanajeshi wa Russia na kuchukua jukumu la kutoa mafunzo kwa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Chad pia ilijiunga na nchi nyingine za Afrika na kutaka Marekani iondowe wanajeshi wake nchini humo. Karibu wanajeshi 1,100 wa Marekani wapo Niger na karibu 100 wapo nchini Chad.
Ni wazi kuwa ombi la kuondolewa wanajeshi wa Marekani katika nchi kama vile Chad na Niger halimaanishi tu kupungua ushawishi wa Marekani barani Afrika, bali pia ni ishara ya mabadiliko makubwa katika mahusiano ya jiografia ya kisiasa. Ni dhahir shahir kuwa mwisho wa uwepo wa kijeshi wa Marekani barani Afrika na katika eneo la Sahel unaweza kusababisha changamoto nyingi kwa sera za kigeni za serikali ya Marekani, ambapo matokeo yake yatakuwa kushindwa Washington kijiopolitiki. Sababu kuu ya ukweli huu ni kwamba mataifa yanayochuana kama vile Russia na China yamedhamiria kuimarisha uwepo wao kijeshi na kiuchumi barani Afrika kwa kutumia fursa ya ombwe la madaraka lililosababishwa na kuondoka kwa wanajeshi wa nchi za Magharibi katika nchi za Kiafrika.
Kwa mfano Kampuni ya Mafuta inayomilikiwa na serikali ya China imetia saini mkataba mkubwa wa kifedha na Niger, ambao pamoja na kutoa fedha kwa serikali ya nchi hiyo, pia unaimarisha nafasi na ushawishi wa China nchini humo.
Aidha inapasa kutiliwa maanani kuwa kuondoka wanajeshi wa Marekani huko Niger na Chad kunaweza kuleta mabadiliko kote barani Afrika ambayo yatazichochea nchi nyingine za Kiafrika kufuata mabadiliko hayo na pia kuimarisha hisia dhidi ya uistikbari na ukoloni wa nchi za Magharibi.