May 21, 2024 07:19 UTC
  • Makomandoo 3 wa US wahusishwa na jaribio la mapinduzi DRC

Makomandoo watatu wa Marekani na raia mmoja wa Uingereza ni miongoni mwa makumi ya watu waliokamatwa na vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakituhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.

Msemaji wa Jeshi la DRC, Brigedia Jenerali Sylvain Ekenge amemtaja mwanasiasa Mkongomani anayeishi Marekani, Christian Malanga kuwa kiongozi wa jaribio hilo la mapinduzi lililotibuliwa.

Amesema Malanga aliuawa katika jaribio hilo lililofeli, na kwamba watu 50 waliokamatwa wakiwemo Wamarekani watatu na Muingereza mmoja wamezuiliwa na wanaendelea kusailiwa na jeshi la DRC.

Vikosi vya jeshi la serikali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo juzi Jumapili vilifanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi dhidi ya rais wa nchi hiyo. Jeshi la DRC limelaani jaribio hilo la kuyumbisha na kuzusha ukosefu wa uthabiti katika taasisi za uongozi nchini humo.

Rais Felix Tshisekedi wa DRC

Tangazo la jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya Kinshasa linakuja kufuatia shambulizi lililolenga makazi ya Naibu Waziri wa Uchumi, Vital Kamerhe, anayetarajiwa kuchukua wadhifa wa Spika nchini DRC katika kitongoji cha Gombe, kilicho karibu na "Ikulu ya Taifa", ambako Rais Felix Tshisekedi anaishi.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) amelaani na kukosoa vikali jaribio hilo la mapinduzi DRC. Moussa Faki Mahamat amesema anafuatilia kwa karibu mambo yanavyoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku akikaribisha habari ya kudhibitiwa wahusika wa jaribio.

 

Tags