Jun 14, 2024 07:10 UTC
  • Kagame alifanyia mabadiliko baraza la mawaziri mwezi mmoja kabla ya uchaguzi mkuu

Rais Paul Kagame wa Rwanda amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri wiki kadhaa kabla ya kufanyika uchaguzi wa Rais nchini humo.

Ripoti kutoka Kigali zinasema, mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa urais, Rais Paul Kagame amefanya mabadiliko katika serikali yake, haswa katika wizara za Mambo ya Nje, Fedha na Mambo ya Ndani, na kumteua mkuu mpya wa upelelezi wa kijeshi.

Paul Kagame (66), ni mgombea anayepewa nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo Vincent Biruta anachukua nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani na Olivier Nduhungirehe, balozi wa zamani wa Rwanda nchini Uholanzi, anachukua nafasi ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni.

Rais Paul Kagame wa Rwanda

 

Marekebisho pia yamefanyika kwa wizara ya fedha na mazingira. Paul Kagame pia amemteua Aimable Havugiyaremye kama mkuu wa idara ya Ujasusi na Usalama (NISS), huduma za kijasusi za kijeshi, ikiwa ni mara ya kwanza raia kushikilia nafasi hiyo.

Akipewa sifa ya maendeleo ya kuvutia ya Rwanda, bila kumwaga damu baada ya mauaji ya halaiki, Rais Paul Kagame anashutumiwa mara kwa mara kwa kukandamiza uhuru wa kujieleza na kukandamiza upinzani wote. Hata hivyo serikali yake imekkuwa ikikanusha viikali madai ya kukandamiza upinzani au kukiuka haki za binadamu ikisisitiza kwamba, hayana msingi wowote.