Holocaust ya Israel na Marekani kaskazini mwa Ukanda wa Gaza
(last modified Sat, 26 Oct 2024 03:08:58 GMT )
Oct 26, 2024 03:08 UTC
  • Holocaust ya Israel na Marekani kaskazini mwa Ukanda wa Gaza

Hata kama mpango wa majenerali wa utawala ghasibu wa Israel wa kuwaondoa kabisa Wapalestina kaskazini mwa Ukanda wa Gaza haujafanikiwa, lakini utawala huo unashirikiana kwa karibu na Marekani kutekeleza mauaji ya umati ya holocaust katika eneo hilo.

Akizungumzia suala hilo, Philip Lazzarini, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) alisema katika taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa Jumatano usiku kwamba: "Watu wote kaskazini mwa Ukanda wa Gaza wanasubiri kifo na kifo kimegeuka kuwa hatima isiyoepukika kwao."

Watu hawa wamefikia natija kwamba wote wametelekezwa na wako katika hatari ya kupatwa na mauati wakati wowote ule. Afisa huyo mkuu wa UNRWA ameongeza kuwa: 'Watu wengi wa Ukanda wa Gaza wamekusanyika katika sehemu finyu ambayo ni chini ya asilimia 10 ya jumla ya ukanda huo, na takriban watu 400,000 bado wako chini ya mzingiro mkali wa kutisha kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, na msimu wa baridi kali unapozidi kukaribia, maafa bila shaka yataongezeka.'

Katika ripoti yake kuhusu hali mbaya ya watu wa Gaza kaskazini mwa eneo hilo, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa hatua ya jeshi la Israel ya kuhamisha Wapalestina kwa nguvu na kuwaweka njaa kama silaha ya vita katika Ukanda wa Gaza, ni jinai mpya ya kivita.

Mwakilishi wa kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa pia ameonya katika barua kwa viongozi wa umoja huo kwamba zaidi ya watu lakini 4.7 kaskazini mwa Gaza wanakabiliwa na mauaji ya umati yanayoweza kuwapata wakati wowote.

Utawala wa Isreal wawafukuza Wapalestina kwenye makazi yao

Tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba, jeshi la Israeli lilizindua rasmi mpango unaojulikana kama "Mpango wa Majenerali" wa kugeuza eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza kuwa eneo la uzio na kijeshi. Mnamo Oktoba 6, jeshi la Israeli lilitoa taarifa rasmi likiwaamuru watu wote kuhama makazi yao Kaskazini mwa Gaza na kuelekea kusini mwa ukanda huo.

Jeshi la Kizayuni limefunga njia zote za kufikisha misaada ya kibinadamu katika eneo hilo ili kuwasababishia baa la njaa na hatimaye kuwalazimisha wakaazi wa eneo hilo kuhama na kuacha nyumba zao.

Mnamo Novemba 2023, Israel ilianzisha "Korido ya Netsarim" ambayo inatenganisha kikamilifu eneo la kaskazini mwa Gaza na sehemu nyingine za kati na kusini mwa ukanda huo. Hata kama katika kipindi chote cha vita vyake vya maangamizi ya umati dhidi ya Wapalestina utawala wa Kizayuni umetumia kila aina ya silaha katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, lakini katika wiki za hivi karibuni, na kufuatia kutekelezwa mpango unaoitwa kuwa wa majenerali, umekuwa ukitumia silaha mpya kuweza kutekeleza kirahisi mpango wake wa mauaji ya halaiki na kuwahamisha kwa nguvu wakaazi wa kaskazini mwa Gaza.

Silaha hizi ni pamoja na roboti na mapipa ya kulipuka. Roboti hizo hubeba mapipa ya takriban tani moja ya milipuko, ambazo hutembea kati ya nyumba na majengo ya makazi, na kudhibitiwa na wanajeshi kwa mbali. Baada ya kufika kwenye vituo vya mikusanyiko ya Wapalestina na majengo yenye watu wengi, hulipuliwa na wanajeshi hao kwa ajili ya kuwaua kwa umati Wapalestina.

Magadi wa Kizayuni wawakandamiza Wapalestina kwa msaaad wa askarijeshi wa utawala wa Israel

Kulipuliwa nyumba na kudodonshwa mabomu kwenye vichwa vya wakaazi kupitia mashambulio ya anga na makombora ni jinai nyingine ya kivita ambayo hufanywa mara kwa mara na Wazayuni huko Jabalia. Sasa, baada ya kupita siku 21 tangu utawala wa Kizayuni uanze kutekeleza mauaji makubwa ya umati dhidi ya watu wa kaskazini mwa Gaza, vyombo vya habari vya Marekani vimedai kuwa Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, ambaye hivi karibuni alikuwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu, eti aliwafahamisha watawala wa Israel kuhusu wasiwasi wake juu ya "mpango wa majenerali".

Kando na misaada yote ya kifedha, kijeshi na kiusalama ambayo Ikulu ya White House hutoa kwa jeshi la Kizayuni kwa ajili ya kuendeleza jinai na mauji ya umati dhidi ya Wapalestina, mojawapo ya njia zisizojulikana sana za misaada ya Marekani kwa utawala huo ni kuupa wakandarasi binafsi wa Kimarekani, ambao ni mamluki maalumu wa kijeshi.

Baada ya kuanza mashambulizi ya nchi kavu ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza, matatizo mengi na mapungufu makubwa ya jeshi la Wazayuni kwa mara nyingine tena yamewafanya Wamarekani wafikirie njia za kuwatuma tena mamluki hao wa kijeshi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Hatari ya hatua hiyo kama si kubwa zaidi, basi si ndogo kuliko ya mabomu ya tani 1.5 ya Marekani yanayodondoshwa kila siku kwenye vichwa vya Wapalestina wasio na ulinzi wa Gaza na pia raia wa Lebanon.