Jun 14, 2024 07:29 UTC
  • ANC: Tumefikia makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa

Chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC, kimetangaza kuwa, kimefikia makubaliano na vyama vingine ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Makubaliano hayo ni natija ya mazungumzo ya ushirikiano baada ya ANC kushindwa kupata viti vya kutosha bungeni katika uchaguzi uliofanyika mwezi Mei. 

Katibu Mkuu wa ANC, Fikile Mbalula amewaambia waandishi wa habari kwamba, serikali ijayo ya Afrika Kusini itakuwa ya sera za mrengo wa kati baada ya vyama vya mrengo mkali wa kushoto kukataa mazungumzo ya kujiunga na serikali.

Mbalula ameeleza kuwa, wamefikia makubaliano chini ya msingi wa pande zote kuridhia haja ya kufanya kazi pamoja.

Duru za ndani ya makubaliiano hayo zinaeleza kuwa, makubaliano hayo yumkini yakamuwezesha Rais Cyril Ramaphosa kuchaguliwa kwa muhula wa pili wakati bunge jipya litakapofanya kikao cha kwanza baadae leo mjini Cape Town.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini

 

Mbalula ameuelezea muungano uliopatikana kuwa utaunda serikali ya umoja wa kitaifa na utavijumuisha vyama vya Democratic Alliance (DA), Chama kinachopigania maslahi ya jamii ya Wazulu cha Inkatha Freedom (IFP) na vyama vingine viwili vidogo kile cha mrengo wa kati kushoto cha United Democratic Movement na cha mrengo mkali wa kulia cha Freedom Front Plus (FF+).

Chama cha ANC, ambacho kiliwahi kuongozwa na mwanasiasa wa kimataifa Nelson Mandela, kilitawala siasa za Afrika Kusini kwa miongo mitatu iliyopita hadi kilipopoteza wingi wake katika uchaguzi wa taifa na wa majimbo tarehe 29 Mei.

Chama hicho, ambacho kilikuwa kikipata zaidi ya 60% katika chaguzi zote tangu 1994, isipokuwa 2019, wakati ushindi wake ulipopungua hadi 57.5%, kilipata 40.18% tu ya kura katika uchaguzi wa mwaka huu.