Kikao cha wiki moja cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kinaendelea Nairobi Kenya
(last modified Tue, 18 Jun 2024 09:49:47 GMT )
Jun 18, 2024 09:49 UTC
  • Kikao cha wiki moja cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kinaendelea Nairobi Kenya

Wajumbe wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walioanza mkutano wa wiki moja jana Jumatatu huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya, wameendelea na mkutano huo kwa siku ya pili mfululizo leo Jumanne kwa ajili ya kuandaa ramani ya kina ya kushirikishwa Somalia katika umoja huo wa kikanda.

Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Mueni Nduva, ambaye alifungua rasmi mkutano huo jana, aliangazia muktadha wa kihistoria na umuhimu wa kuwa na ramani ya kuiunganisha Somalia katika jumuiya hiyo. Alisema: Somalia ilipata uanachama kamili wa EAC mwezi Machi baada ya kuweka rasmi hati yake ya kuridhia Mkataba na Hati inayounda EAC.

Kuingia Somalia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutainufaisha nchi hiyo na miradi ya miundombinu ya kikanda kama vile barabara, reli na mitandao ya nishati. 

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Nduva amesema: Baada ya kukamilisha muongozo na ramani ya njia, itatumika kama marejeo ya kimkakati ya kusawazisha ratiba na kuhamasisha rasilimali kwa ufanisi katika upeo wa ukanda huo mzima.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Katibu Mkuu wa EAC amesema: Miradi hii inalenga kuboresha mawasiliano, kuimarisha usafiri, kukuza biashara ya kikanda na hatimaye kusaidia maendeleo ya kiuchumi ya Somalia.

Kwa upande wake, Abdusalam H. Omer, mjumbe maalumu wa rais wa Somalia, ameelezea matumaini yake kuhusu ushirikiano wa wanachama wote katika kuunda muongozo wa kuhakikisha Somalia  inakuwa na ushirikiano mzuri ndani ya jumuiya hiyo.

Amesema: "Somalia itaendelea kuwa imara katika dhamira yake ya kutimiza malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kukuza umoja, ustawi na amani katika ukanda mzima."