Walibya wataka kuhitimishwa mizozo ili uchaguzi ufanyike
(last modified Thu, 20 Jun 2024 11:08:14 GMT )
Jun 20, 2024 11:08 UTC
  • Walibya wataka kuhitimishwa mizozo ili uchaguzi ufanyike

Umoja wa Mataifa umetangaza kuuwa, raia wa Libya wanataka mipasuko nchini mwao ikome na wanasiasa wanaohasimiana waandae uchaguzi iili kuikwamua nchi hiyo katika kinamasi cha mkwamo wa uongozi.

Hayo yameelezwa na Stephanie Koury Naibu mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ambaye ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Walibya kutoka matabaka mbalimbali na maeneo yanayohasimiana wamechoshwa na migawanyiko inayoshuhudiwa nchini mwao. Amesema, wananchi wa Libya wanataka wadau wa siasa wautafutie ufumbuzi mkwamo wa muda mrefu wa kisiasa nchini humo na wakubaliane kuandaa uchaguzi wa kitaifa.

Koury ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, amekuwa akikutana na viongozi wa kisiasa, wawakilishi wa mashirika ya kijamii na asasi za kiraia, wasomi, makundi ya wanawake, viongozi wa kijeshi na wengine katika maeneo yanayohasimiana ya mashariki na magharibi kuwasikiliza maoni yao.

Libya imetumbia katika vita vya ndani tangu 2011 baada ya kiongozi wake Kanali Muammar Gaddafi kuondolewa madarakani

 

Libya imekuwa katika hali ya ukosefu wa amani na mivutano ya kisaisa tangu baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Hali ya kisiasa na tofauti za mitazamo zimepelekea nchi hiyo kukosa serikali kuu yenye nguvu kwa ajili ya kuandaa uchaguzi wa kumchagua rais wa nchi hiyo.

Ijapokuwa mashirika ya kimataifa yamefanya jitihada nyingi kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa Libya na makundi ya kisiasa kutangaza kuwa tayari kuandaa uchaguzi, lakini kivitendo tofauti za maoni zimekuwa zikizidisha mzozo wa kisiasa na hivyo kutia dosari uwezekano wa kufanyika uchaguzi huo.