Jun 21, 2024 11:56 UTC
  • Umoja wa Afrika kuchunguza ombi kuhusu wanajeshi wa ATMIS Somalia

Umoja wa Afrika (AU) umesema kuwa, unalichunguza ombi la Somalia la kupunguza kasi ya kuondoka vikosi vya kulinda amani vya umoja huo (ATMIS) vyenye jukumu la kupambana na kundi al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa al-Qaida.

Baada ya kikao kilichofanyika siku ya Alkhamis (Juni 20) mjini Addis Ababa, Ethiopia, mmoja wa wanadiplomasia wa Umoja wa Afrika alisema, huenda baraza lake la amani na usalama likaridhia ombi la Somalia na kuchelewesha kwa miezi kadhaa mchakato wa kuondoka vikosi vya ATMIS.

Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika (AU) nchini Somalia (ATMIS) kimetangaza kwamba kimekabidhi kambi ya kijeshi ya Barire kwa vikosi vya usalama vya Somalia ikiwa ni kuashiria kuanza awamu ya tatu ya kuondoa wanajeshi wake nchini humo.

Ujumbe wa AU uliondoa wanajeshi 5,000 nchini Somalia na kukabidhi kambi 17 za kijeshi kwa Vikosi vya Usalama vya Somalia wakati wa awamu ya kwanza na ya pili ya kuondoka kijeshi nchini humo, zoezi ambalo lilikamilika mwaka jana 2023.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

 

Awamu ya tatu ya kupunguzwa wanajeshi wa ATMIS inafanyika kwa mujibu wa maazimio nambari 2628 (2022), 2670 (2022), na 2710 (2023) ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo yanaiamuru ATMIS kuondoa wanajeshi 4,000 ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Juni.

Tangu mwaka 2007, magaidi wa al-Shabaab wamekuwa wakipigana na serikali ya Somalia na Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini humo (ATMIS) lakini mashambulizi yake yamekuwa ya kifeli hasa baada ya genge hilo kufurushwa kwenye miji mikubwa ya Somalia na kubakia katika baadhi ya vijiji ambako inavitumia kuendesha mashambulizi ya kuvizia na ya chini kwa chini.