Jun 21, 2024 12:18 UTC
  •  WFP: Msaada wa chakula waongezeka Darfur lakini hautoshi

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema kuwa, jimbo la Darfur limeshuhudia ongezeko la msaada wa chakula unaohitajika, lakini likaonya kwamba kiwango hicho bado hakitoshi kuzuia baa la njaa.

Taarifa iliyotolewa na WFP imesema kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2024, misafara mitano iliyobeba karibu tani 5,000 za msaada wa chakula imevuka kutoka nchi jirani ya Chad hadi eneo la Darfur linalokumbwa na mzozo wa kijeshi.

Mkuu wa mawasiliano katika ofisi ya WFP nchini Sudan, Leni Kinzli, ameziambiia duru za habari kwamba, usambazaji wa chakula unaendelea katikati mwa Darfur na magharibi mwa jimbo hilo "na kwamba hiyo ni hatua ya dharura ili kuepusha baa la njaa kote nchini humo.

Pamoja na hayo, Shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa limeonya kuhusu hatari ya njaa huko Darfur iwapo pande zinazozozana hazitaruhusu msaada kuingia katika eneo hilo la magharibi mwa Sudan.

 

WFP inasema kuongezeka mapigano katika mji mkuu wa Darfur Kaskazini, El Fasher, kunazuia juhudi za kupeleka msaada muhimu wa chakula katika eneo hilo.

Raia katika mji huo na eneo pana la Darfur tayari wanasumbuliwa na kiwango kikubwa cha njaa, lakini uwasilishaji wa msaada wa chakula umekuwa wa kusuasua kutokana na vikwazo vya ukiritimba na mapigano yanayoendelea katika maeneo hayo.

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF)  linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.