Wanamgambo wa CODECO waua watu 23 mashariki mwa DRC
Zaidi ya watu 23 wanaripotiwa kuuawa na waasi wa kundi la CODECO katika vijini kadhaa kwenye jimbo lenye utajiri mkubwa wa dhahabu la Ituri kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ingawa chanzo cha mashambulizi hayo hakijabainishwa, lakini vurugu za wanamgambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinahusishwa na ushindani wa muda mrefu wa kuwania ushawishi na utajiri wa rasilimali za madini katika eneo hilo.
Kundi la wanamgambo linalojulikana kama Ushirika wa Maendeleo ya Kongo (CODECO), moja kati ya makundi mengi yenye kujihami kwa silaha, ndilo linalotajwa kuhusika na mauaji haya ya karibuni kabisa.
Kwa mujibu wa ripoti ya ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa wa Kongo, iliyotolewa hivi karibuni ni kuwa, CODECO, kundi la ADF na wanamgambo wengine wanahusika katika matukio mengi ya mauaji ya raia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Genge la ADF ni maarufu kwa vitendo vyake vya mauaji ya kutisha katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri ambayo yanashuhudia machafuko ya miaka mingi huku serikali ikishindwa kuwadhaminia wananchi usalama wao.
Tangu mwezi Novemba 2021 hadi hivi sasa, wanajeshi wa Uganda pamoja na wenzao wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wamekuwa wakishirikiana katika operesheni za pamoja za kupambana na genge hilo la waasi mashariki mwa DRC.
Hii ni katika hali ambayo mwezi uliopita wa Mei, jeshi la Uganda liltangaza kuwa, limemkamata kamanda wa kundi la waasi la ADF ambaye ni mtaalamu wa kutengeneza mabomu yaliyokuwa yanatumiwa na genge hilo kufanya mashambulizi mabaya dhidi ya raia.