Spika Qalibaf: Iran itatumia vita na diplomasia kutetea haki za watu wake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139008-spika_qalibaf_iran_itatumia_vita_na_diplomasia_kutetea_haki_za_watu_wake
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf anasema mkakati wa nchi wa kukomesha uchokozi wa Marekani na Israel ni kutumia vita na diplomasia kwa wakati mmoja ili kutetea haki za taifa la Iran.
(last modified 2026-06-09T12:24:37+00:00 )
Jun 09, 2026 12:21 UTC
  • Mohammad Baqer Qalibaf
    Mohammad Baqer Qalibaf

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf anasema mkakati wa nchi wa kukomesha uchokozi wa Marekani na Israel ni kutumia vita na diplomasia kwa wakati mmoja ili kutetea haki za taifa la Iran.

Katika ujumbe wa sauti uliotolewa kwa taifa la Iran jana Jumatatu, Qalibaf alisema kwamba Iran iko tayari kuanza tena shughuli zake za kijeshi mara moja ili kujibu ukiukaji wa Marekani na Israel wa usitishaji mapigano uliotangazwa mapema Aprili.

Matamshi yake yamekuja baada ya Iran kufanya mashambulizi ya makombora dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kujibu ukiukaji wake wa masharti ya kusitisha mapigano, ambayo pia yanajumuisha kusitishwa uhasama nchini Lebanon.

Operesheni hiyo imefanyika licha ya juhudi zinazoendelea za kufikiwa makubaliano kati ya Iran na Marekani ambayo yanaweza kukomesha kabisa uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran ulioanza mwishoni mwa Februari mwaka huu.

Qalibaf, ambaye ameongoza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja baina ya Iran na Marekani, amesema Tehran imekuwa makini katika harakati zake za diplomasia ili kukomesha uchokozi huo.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba majibu ya kijeshi ya Iran kwa ukiukaji wa Marekani wa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ghuba ya Uajemi na dhidi ya mashambulizi ya Israel nchini Lebanon pia ni sehemu thabiti ya mkakati wa Iran wa kufikia malengo yake katika mapambano ya sasa.

"Kama tutaitazama diplomasia kama mazungumzo ya faragha na tabasamu za kidiplomasia, tutashindwa tangu mwanzo. Na tukitegemea tu shughuli za kijeshi na vita, hatuwezi kutetea haki zetu kikamilifu," Qalibaf amesema katika ujumbe wake kwa taifa.

Ameongeza kuwa, kuongezeka mapigano hivi karibuni dhidi ya Marekani na utawala wa Israel kulitokana na kuendelea vikwazo vya Marekani dhidi ya biashara ya baharini ya Iran na mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon.

"Ilikuwa jambo la kawaida kwetu kutoa jibu madhubuti kwa ajili ya kutetea haki za taifa la Iran," amesema Qalibaf na kupongeza vikosi vya jeshi la kwa kufanya kazi kwa nguvu kamili.

Kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya kukomesha vita na Marekani ameweka wazi kwamba Tehran haina imani na Marekani inaposhiriki katika mazungumzo ya kidiplomasia na Washington. "Lengo letu ni kukomesha vita na kurejesha usalama wa kudumu, si kurekebisha uhusiano na Marekani," amesisitiza Spika Qalibaf.