Araghchi afanya mazungumzo ya kidiplomasia kuhusu uchokozi wa Israel
-
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, amefanya mfululizo wa mazungumzo kwa njia ya simu na baadhi ya mawaziri wenzake wa maeneo mbali mbali duniani pamoja na kamanda wa jeshi, kufuatia hatua ya Iran kujibu ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya usitishaji mapigano nchini Lebanon unaotekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Usiku wa Jumapili, Araghchi alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper; Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan; Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Field Marshal Asim Munir; Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean‑Noël Barrot; Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani; Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty; Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Fuad Hussein; pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud.
Mazungumzo hayo yalifanyika baada ya Iran kutangaza kuchukua hatua za kujibu dhidi ya utawala wa Israel kufuatia mashambulizi yake katika vitongoji vya kusini mwa Beirut na mashambulizi yanayoendelea kusini mwa Lebanon.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Araghchi amesisitiza msimamo wa Tehran kwamba usitishaji mapigano haupaswi kugawanywa kati ya maeneo tofauti ya mzozo. Ukiukaji wowote unaofanywa na utawala wa Israel nchini Lebanon unachukuliwa kuwa ni uvunjaji wa makubaliano yote kwa ujumla wake, jambo ambalo, kwa mtazamo wa Iran, linawapa wajibu kamili na wa moja kwa moja utawala huo wa Kizayuni pamoja na wanaouunga mkono nchini Marekani.
Maafisa waandamizi wa Iran wamesisitiza kwamba hatua zilizochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu zililenga kutoa jibu kwa madhumuni ya kuzuia uchokozi zaidi na kulinda usalama wa mhimili wa muqawama.
Araghchi pia amesisitiza dhamira thabiti ya Iran katika kudumisha amani na utulivu katika eneo la Asia Magharibi, huku akibainisha umuhimu wa kusitishwa kwa vitendo vya uchochezi vya utawala ghasibu wa Israel.
Katika mazungumzo hayo ya simu, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran alibadilishana mawazo kuhusu juhudi za kuimarisha usitishaji mapigano na kuzuia ongezeko lolote la mvutano linaloweza kuchochewa na kile alichokitaja kama uchokozi wa Kizayuni.
Aidha ametaja mchango wa Pakistan kuwa chanya katika juhudi pana za kidiplomasia, hasa katika kuwezesha hatua za kupunguza mvutano kati ya Iran na Marekani, na akaonyesha kuthamini ushiriki wa Ankara katika masuala ya kuimarisha uthabiti wa kikanda.
Kwa upande wake, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Marekani inabeba dhima ya kushadidi mvutano katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati), akisisitiza kwamba utawala wa Israel hauchukui hatua zozote bila uratibu wa awali na Marekani. Esmaeil Baghaei ameyasema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran siku ya Jumatatu.
Amesema hatupaswi kusahau kwamba Marekani ndiyo ilianzisha vita dhidi ya Iran ili kuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel.