Haftar akanusha kukipatia silaha kikosi cha RSF kinachopigana na serikali ya Sudan
-
Khalifa Haftar
Serikali ya mashariki mwa Libya, ambayo haitambuliwi na jamii ya kimataifa imekanusha taarifa zinazodai kwamba, imekuwa ikiwapatia silaha wapiganaji wa RSF wanaoongozwa na Hamdan Dagalo katika vita vya ndani nchini Sudan.
Serikali hiyo imezungumzia rasmi na kwa mara ya kwanza kuhusu tuhuma za kuhusika katika vita vya Sudan. Imekanusha, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, shutuma mpya za Jenerali al-Burhan, zilizozitolewa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Sudan, aliye karibu na Jenerali al-Burhan. Mbabe wa kivita wa Libya Khalifa Haftar anatuhumiwa kutuma silaha na risasi kwa wapiganaji wa RSF nchini Sudan.
Hata hivyo serikali ya mashariki mwa Libya imeelezea kushangazwa kwake na kukanusha kuhusika kwa namna yoyote na vita vinavyoendelea nchini Sudan, ikizituhumu pande hizo mbili zinazopigana kwa kufanya uhalifu unaolingana na mauaji ya kikabila.
Suala la uhusiano kati ya Marshal Haftar na RSFinayoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo limekuwa mjadala mkali tangu kuanza kwa vita nchini Sudan.
Hivi karibuni balozi na mwakilishi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa aliushutumu Umoja wa Falme za Kiarabu kusaidia wapiganaji wa RSF kupitia wanamgambo nchini Chad, Kusini mwa Libya na Afrika ya Kati, akiongeza kuwa Sudan iliwasilisha kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hati kadhaa za kusafiria za Umoja wa Falme za Kiarabu zilizogunduliwa kwenye uwanja wa mapigano mjini Khartoum.
Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana (2023) kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.