Mamia waandamana Senegal wakitaka nchi yao kukata uhusiano wa kidiplomasia na Israel
Mamia ya wananchi wa Senegal wameandamana na kutoa wito kwa nchi yao kukata uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel.
Ripoti zinaeleza kuwa, kulikuwa na mamia ya waandamanaji waliohudhuria maandamano hayo ambao walisisitiza ulazima wa kuchukuliwa hatua madhubuti zaidi za kusitishwa kwa mauaji ya umati katika Ukanda wa Gaza yanayofanywa na utawala ghasibu wa Israel.
"Tunapaswa kuzidisha mashinikizo dhidi ya Israel na waungaji mkono wake ili kusitisha vita mara moja huko Gaza," Seydi Gassama alimwambia mwandishi wa habari wa Iranpress pambizoni mwa maandamano hayo.
Waandamanaji hao wamesisitiza kuwa, serikali ya Senegal inapaswa kukata uhusiano wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel kutokana na utawala huo kutenda mauaji ya kimbari huko Gaza.
Aidha wameitaka jamii ya kimataifa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina wanaotaabika kutokana na athari za vita..
Hayo si maandamano ya kwanza kufanyika nchini Senegal kuitaka serikali ya Dakar isitishe uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel.
Hivi karibuni, wanaharakati wa mashirika ya kiraia nchini Senegal walitoa mwito kwa serikali ya nchi yao kukakata uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel, kutokana na jinai za kivita na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Wanaharakati wa mashirika 19 ya kiraia katika nchi hiyo ya Afrika Maghairibi wameanzisha kampeni ya kuishinikiza serikali ya Dakar kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Tel Aviv kutokana na mashambulizi ya umwagaji damu yanayofanywa na Wazayuni huko Gaza.