Rais Ruto: Niko tayari kuwashirikisha vijana katika suala la muswada wa fedha
Rais wa Kenya William Ruto amesema yuko tayari kuwashirikisha vijana katika juhudi za kulitafutia ufumbuzi suala la muswada wa fedha nchini humo. Msimamo huo wa kiongozi huyo umekuja baada ya kushuhudiwa maandamano makubwa yaliyoitikisa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa siku kadhaa sasa.
Asasi za kiraia na mashirika ya kutetea haki za binadamu yameijia juu polisi ya Kenya kwa tuhuma za kumuua kwa kumpiga risasi mmoja wa waandamanaji wanaopinga mpango wa kuongeza ushuru, kodi na tozo.
Mwanaharakati Rex Kanyike Masai, 29, aliaga dunia hivi karibuni kutokana na majeraha ya risasi, aliyopigwa akishiriki maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha wa 2024 katika barabara ya Moi jijini Nairobi.
Maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha yameshika kasi jijini Nairobi na katika miji mingine mikubwa ya nchi hiyo, huku biashara nyingi zikisalia kufungwa.
Maelfu ya waandamanaji, wengi wao wakiwa ni vijana wa kizazi cha sasa (Gen Z) wamekuwa wakiandamana tokea Jumanne iliyopita, wakimkosoa Rais William Ruto na serikali yake kwa kuwatelekeza vijana kinyume na alivyoahidi katika kampeni zake na manifesto ya Kenya Kwanza.
Wakati huo huo, kinara wa Mawaziri wa Kenya, Musalia Mudavadi, amesema Muswada wa Fedha 2024 lazima upitishwe na kutiwa saini na Rais William Ruto kuwa sheria, akisema kinyume na hivyo itakuwa ni sawa na kuangusha Serikali.
Waandamanaji, wengi wao wakiwa vijana na chipukizi, wanataka muswada huo utupiliwe mbali, wala sio kukarabatiwa, wakisema kwamba licha ya mapendekezo ya kuondoa baadhi ya ushuru, bado kuna ushuru kwenye vipengele vingine ambao utafanya maisha kuwa magumu kuliko yalivyo sasa.