Jun 26, 2024 11:50 UTC
  • Makumi ya askari wauawa katika shambulio la kigaidi Niger

Askari wasiopungua 20 wa jeshi la Niger wameuauwa katika shambulio la 'muungano wa makundi ya kigaidi' magharibi mwa nchi hiyo.

Wizara ya Ulinzi ya Niger imesema katika taarifa kuwa, magaidi waliokuwa wamejizatiti wa silaha walifanya ukatili huo baada ya kushambulia mkusanyiko wa maafisa wa usalama na ulinzi katika kijiji cha Tassia kilichoko katika eneo la Tillaberi, katika mpaka wa nchi hiyo na Mali na Burkina Faso.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mbali na wanajeshi 20 wa Niger na raia mmoja kuuawa katika hujuma hiyo ya jana Jumanne, lakini pia askari wengine tisa wamejeruhiwa.

Luteni Jenerali Salifou Mody, Waziri wa Ulinzi wa Niger sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia askari waliouawa na kuwatakia afueni ya haraka majeruhi, amelihakikishia taifa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo vitaendelea kupambana kwa nguvu zote kulinda amani, usalama, uthabiti na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.

Wanajeshi wa Niger wakishika doria

Baraza la kijeshi la Niger limetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo Jumatano, kufuatia maafa ya shambulio hilo linalodaiwa kufanywa na 'muungano wa makundi ya kigaidi'.

Bendera zitapepea nusu mlingoti katika kipindi hicho cha maombolezo. Hadi sasa hakuna kundi lolote la kigaidi lililodai kuhusika na shambulio hilo.

Niger, ambayo ni moja ya nchi masikini zaidi duniani, imekuwa katika vita vikali na makundi ya kigaidi kama Boko Haram, Daesh (ISIS) na kundi la kigaidi la Al-Qaeda kwa miaka kadhaa sasa.

 

Tags