Jun 27, 2024 02:59 UTC
  • Misri yaikosoa Israel kwa kuiba misaada ya kibinadamu ya Wapalestina

Waziri wa Mambo ya Nje ya Misri amekosoa hatua ya utawala haramu wa Israel ya kupora na kuzuia kuingizwa na kusambazwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, kupitia kivuko cha Rafah.

Sameh Shoukry ameeleza haya katika mazungumzo ya simu na Sigrid Kag, Mratibu Mkuu wa Masuala ya Binadamu wa Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, utawala haramu wa Israel unaendeleza vikwazo visivyo halali vya kuzuia kupelekwa misaada ya kibinadamu Gaza.

Waziri huyo ameitaka Israel iheshimu sheria za kimataifa na iondoe vizuizi hivyo katika usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa raia wa eneo hilo lililo chini ya mzingiro. Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Misri ameeleza bayana kuwa, misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Gaza haitoshi, na eneo hilo linakaribia kutumbikiia katika maafa makubwa ya kibinadamu.

Amesema kivuko cha Rafah kiko wazi tangu mwanzo wa mgogoro wa Ukanda wa Gaza na hakijafungwa katika hatua yoyote ile, lakini utawala wa Kizayuni wa Israel unazuia misaada kuingia Gaza kupitia njia mbalimbali.

Waziri wa Mambo ya Nje ya Misri, Sameh Shoukry

Wazayuni wanapora misaada ya kibinadamu ya Wapalestina katika hali ambayo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeendelea kusisitiza kuwa, wajibu wa mamlaka ya Israel ni kuandaa mazingira ya upelekaji misaada bila ya vizingiti.

Jeshi la utawala wa Kizayuni mara kadhaa limefanya uvamizi na mashambulio ya nchi kavu dhidi ya mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza na kukifunga kivuko cha mji huo cha baina ya Gaza na Misri, ambacho kinachukuliwa kuwa moja ya njia muhimu zaidi za kupitishia misaada ya kibinadamu kuelekea eneo hilo la Palestina.

 

Tags