Jul 03, 2024 06:44 UTC
  • Watu 40 wauawa katika shambulio la wabeba silaha Mali

Makumi ya watu wameuawa katika shambulio la genge la wabeba silaha, lililolenga kijiji kimoja cha katikati mwa Mali.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Reuters, maafisa wa serikali ya Mali walitangaza habari hiyo jana Jumanne na kuongeza kuwa, raia wasiopungua 40 wameuawa katika shambulizi hilo lililofanywa na genge la wanamgambo wasiojulikana na waliokuwa wamejizatiti kwa silaha.

Maafisa wa serikali ya Mali wamesema kuwa, idadi ya wahanga wa shambulio hilo la 'kigaidi' dhidi ya wakazi wa kijiji cha Djiguibombo katika jimbo la Mopti yumkini ikaongezeka, kwa sababu waliojeruhiwa ni watu wengi sana.

Meya wa Bankass, Moulaye Guindo ameiambia Reuters kuwa, "Lilikuwa shambulio la kuogofya, watu waliojizatiti kwa silaha walishambulia kijiji na kuanza kuwafyatulia watu risasi ovyo."

Hali tete ya usalama Mali

Shambulio hilo linaonekana kuwa la ulipizaji kisasi, kwani limejiri wiki wiki chache baada ya jeshi la Mali kutangaza kumuua Abu Huzeifa, almaarufu Higgo, mmoja wa vinara wakuu wa magaidi katika eneo la Sahel, magharibi mwa Afrika, wakati wa operesheni katika eneo la Indelimane katika eneo la kaskazini la Menaka karibu na mpaka wa nchi hiyo na Niger.

Aidha haya yameripotiwa wiki chache baada ya makumi ya raia wengine kuuawa katika shambulio jingine la kigaidi lililotokea kwenye kijiji kimoja katika eneo hilo la Mopti la katikati mwa nchi hiyo.

 

Tags