Rais Ruto aagiza kutazamwa upya nyongeza ya mishahara ya serikali
-
Rais William Ruto
Mapendekezo ya nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa Serikali na wawakilishi wa Bunge la Kenya hayatatekelezwa baada ya Rais William Ruto wa nchi hiyo kuagiza kuangaliwa upya kwa mipango hiyo kufuatia malalamiko ya umma.
Rais Ruto ametoa agizo hili wiki moja baada ya Kenya kuathiriwa na maandamano makubwa yaliyomlazimisha Rais kuuweka kando Mswada wa Fedha wa 2024 uliokuwa umejumuisha nyongeza ya kodi.

Lyn Mengich, Mwenyekiti wa Tume ya Mishahara na Malipo ya Kenya (SRC) jana alieleza kuwa tume hiyo itazuia nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa serikali kutokana na hali halisi ya sasa ya uchumi.
Awali tume ya SRC ilikuwa imependekeza nyongeza ya mshahara kwa asilimia 2 na 5 kwa maafisa wote wa serikali wakiwemo majaji. Baada ya pendekezo hilo, wananchi walianza kuhoji ni vipi mishahara ya wanasiasa, wakiwemo magavana, inaweza kupandishwa wakati nchi iko katika mgogoro wa kifedha?
Rais Ruto aliachana na mipango ya kuongeza ushuru baada ya waandamanaji kulalamika kuwa hawana uwezo wa kutoa fedha hizo kwani tayari wanaelemewa na ongezeko kubwa la gharama ya maisha.
Wakenya wengi wanasema kuwa serikali inapasa kubana matumizi yake; suala ambalo Rais William Ruto ameahidi kulifanyia kazi.