Rwanda: Tumezingatia nia ya Uingereza ya kusitisha mpango tata wa uhamiaji
Rwanda jana ilisema kuwa imetilia maanani nia ya serikali ya Uingereza ya kusimamisha mpango tata wa uhamiaji ambao ulisainiwa na nchi mbili hizo kwa lengo la kuwazuia wahamiaji haramu kuingia Uingereza kupitia mfereji wa maji unaozitenganisha nchi mbili za Uingereza na Ufaransa kwa kutumia boti ndogo za usafiri.
Rwanda na serikali ya awali ya kihafidhina ya Uingereza zilitia saini makubaliano mwezi Aprili 2022 ili kufanikisha kutumwa Rwanda baadhi ya wahamiaji waliowasili Uingereza kupitia mfereji huo wa maji kati ya nchi hiyo na Ufaransa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, Keir Starmer alisema katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari kuwa hatoendelea na mpango mkuu wa serikali ya awali ya kihafidhina kuwafukuza wahamiaji na kuwapeleka Rwanda.
"Sijajiandaa kuendelea na mpango huo tata", amesema Keir Starmer.
Kwa upande wake msemaji wa serikali ya Rwanda ameeleza kuwa Kigali inaunga mkono kikamilifu upande wake wa makubaliano hayo, na imejitolea kuutafutua suluhu mgogoro wa kimataifa wa wahamiaji, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wakimbizi na wahamiaji wanaoingia nchini humo wanakuwa salama, wanahudumiwa kwa misingi ya kiutu na kupatiwa fursa mbalimbali.
Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Rishi Sunak alikuwa akisisitiza juu ya mpango huo wa "kusimamisha boti" zinazovuka mfereji wa maji unaotenganisha Uingereza na Ufaransa ili kufanikisha mpango wenye utata wa kuwafukuza na kuwapeleka Rwanda licha ya upinzani mkubwa wa makundi ya haki za binadamu na maamuzi ya mahakama, lakini chama cha Labour kiliahidi kwamba kitaweka kando mpango huo.
Itakumbukwa kuwa Mahakama Kuu ya Uingereza ilitoa uamuzi kuwa mpango huo wa wahamiaji ni kinyume na sheria.