Rwanda yaishtaki serikali ya Uingereza kwa kukiuka makubaliano ya wahamiaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135986-rwanda_yaishtaki_serikali_ya_uingereza_kwa_kukiuka_makubaliano_ya_wahamiaji
Rwanda imeishtaki serikali ya Uingereza kuhusu makubaliano ya wahamiaji ambayo London imeyatelekeza yapata miaka miwili iliyopita.
(last modified 2026-01-28T07:42:55+00:00 )
Jan 28, 2026 07:42 UTC
  • Rwanda yaishtaki serikali ya Uingereza kwa kukiuka makubaliano ya wahamiaji

Rwanda imeishtaki serikali ya Uingereza kuhusu makubaliano ya wahamiaji ambayo London imeyatelekeza yapata miaka miwili iliyopita.

Keir Starmer, Waziri Mkuu wa Uingereza ametelekeza makubaliano hayo yaliyofikiwa kati ya nchi mbili ambayo yalisainiwa na serikali ya wakati huo alipoingia mamlakani mwezi Julai mwaka juzi. 

London iliripotiwa kuilipa Kigali pauni milioni 240 sawa na dola milioni 330.9 kabla ya makubaliano hayo kutelekezwa.

Rwanda imesema kuwa mwezi Novemba mwaka juzi, Uingereza ilitaka iachane na malipo mawili ya pauni milioni 50 ambayo Rwanda ilipaswa kulipwa mwezi Aprili 2025 na Aprili mwaka huu ikisema kuwa inafanya hivyo kwa kutarajia kusitishwa rasmi mkataba huo.

Rwanda ilieleza kuwa inaweza kukubali mipango hiyo iwapo mkataba huo utakatishwa, madhali masharti mapya ya kifedha yatajadiliwa na kukubaliwa.

Hata hivyo majadiliano kati ya Rwanda na Uingereza hatimaye hayakufanyika na kiasi hicho cha fedha kinapaswa kulipwa kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Kigali iliripoti kesi hiyo katika Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi yenye makao yake Uholanzi Novemba mwaka jana baada ya Uingereza kuweka wazi kuwa haina nia ya kufanya malipo mengine kwa mujibu wa mkataba huo.

Rwanda inamtuhumu Waziri Mkuu wa Uingereza kuwa ametangaza kwamba makubaliano hayo yamekufa na kuzikwa bila ya kuitaarifu kwanza Kigali.