Serikali ya Sudan Kusini: Hatuko vitani licha ya mapigano makali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135988-serikali_ya_sudan_kusini_hatuko_vitani_licha_ya_mapigano_makali
Serikali ya Sudan jana ilitangaza kuwa haiko vitani licha ya mapigano makali yanayoendelea dhidi ya waasi katika siku za karibuni.
(last modified 2026-01-28T07:47:07+00:00 )
Jan 28, 2026 07:47 UTC
  • Wanajeshi wa Sudan Kusini
    Wanajeshi wa Sudan Kusini

Serikali ya Sudan jana ilitangaza kuwa haiko vitani licha ya mapigano makali yanayoendelea dhidi ya waasi katika siku za karibuni.

Umoja wa Mataifa umesema mapigano hayo yanajiri kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu kabla ya kufikiwa makubaliano ya amani mwaka 2018.

Mapigano kati ya makundi yanayomuunga mkono Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na mpinzani wake wa muda mrefu, Riek Machar yalizuka mwishoni mwa Disemba mwaka jana katika Jimbo la Jonglei, kaskazini mwa mji mkuu, Juba.

Ateny Wek Ateny Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amesema kuwa operesheni ya usalama inayoendelea kaskazini mwa Jimbo la Jonglei ni hatua halali na muhimu inayolenga kusitisha kusonga mbele harakati za waasi, kurejesha utulivu wa umma na kuwalinda raia.

Vikosi vya Rais Kiir na wanamgambo watiifu kwa aliyekuwa makamu wake wa kwanza, Machar vilipigana vita vikali kuanzia mwaka 2013 hadi 2018. 

Mnamo Septemba mwaka huo, pande mbili zilifikia makubaliano ya amani yaliyojulikana kama "Mkataba Uliohuishwa wa Utatuzi wa Migogoro katika Jamhuri ya Sudan Kusini", (R-ARCSS).

Makubaliano hayo yalipelekea kuundwa serikali ya umoja ambayo mwaka uliopita ilikabiliwa na mtikisiko mkubwa.

Riek Machar amefukuzwa katika serikali ya umoja wa kitaifa na sasa anakabiliwa na kesi ya jinai dhidi ya binadamu. 

Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amesisitiza kuwa makubaliano ya amani ya nchi hiyo hayajasambaratika. 

"Serikali inatoa wito kwa harakati ya SPLM/A kusitisha mara moja hatua za uhasama," amesema Ateny Wek Ateny.