MONUSCO yawarejesha nyumbani waasi 15 wa zamani wa Rwanda kutoka Kongo
-
Askari wa kikosi cha MONUSCO
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) kimeripoti kuwa kimewarejesha nyumbani Wanyarwanda 34, wakiwemo wapiganaji 15 wa zamani wa kundi la waasi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).
Redio ya Umoja wa Mataifa nchini Kongo imetangaza kuwa zoezi hilo limefanywa kupitia kitengo cha MONUSCO cha upokonyaji silaha na uhamishaji na kwamba waliorejeshwa ni pamoja na watu 19 wa familia za waasi wa zamani. Wapiganaji wa zamani 33 wanaifanya jumla ya watu waliorejeshwa Rwanda kutoka Kongo kufikia 60.
Katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la wanaojisalimisha kwa hiari miongoni mwa waasi wa Rwanda katika viunga vya Goma katika jimbo la Kivu Kaskazini kufuatia kutekwa mji huo na waasi wa M23 mwaka jana.
Karibu watu 300 wamerejeshwa makwao tangu mwaka jana chini ya programu ya upokonyaji silaha.
Watu hao wamerejeshwa makwao kufuatia makubaliano ya amani yaliyosainiwa na Kongo na Rwanda mwezi Juni mwaka jana mjini Washington, Marekani kwa lengo la kurejesha amani mashariki mwa Kongo.
Waasi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) wamekuwa nchini Kongo kwa miongo kadhaa sasa na bado wanafanya harakati katika maeneo ya Masisi, Rusthuri na Walikale mashariki mwa nchi hiyo.
Kikosi cha MONUSCO kimesema kuwa kimeimarisha zoezi la uhamasishaji ili kuhakikisha waasi wanajisalimisha kwa hiari na kurejeshwa makwao.