Makumi ya watu wauawa DRC na magaidi wenye mfungamano na ISIS
Wanamgambo wanaohusishwa na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) wamewaua raia wasiopungua 22 katika kijiji kimoja katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa na viongozi wa asasi za kiraia.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na Reuters imesema wanamgambo hao walishambulia kijiji cha Apakolu, yapata kilomita 25 (maili 15) kaskazini magharibi mwa Eringeti katika eneo la Irumu mkoani Ituri, Jumapili jioni, na kuwateka nyara idadi kadhaa isiyojulikana ya watu.
Christophe Munyanderu, mkuu wa kundi la kutetea haki za binadamu linalojulikana kwa kifupi kama CRDH, lenye makao yake Irumu, amesema raia 25 wameuawa, wakiwemo wanaume 15 ambao miili yao ilipatikana ndani ya nyumba na wengine saba kando ya barabara.
Washambuliaji hao walitambuliwa kama wanachama wa Allied Democratic Forces (ADF), kundi lenye silaha la Uganda linaloendesha harakati zake mashariki mwa Kongo DR, na ambalo linatambuliwa na genge la kigaidi la ISIS (Daesh) kama mshirika.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema shambulio la Jumapili huko Apakolu limekuja siku mbili baada ya wapiganaji wa ADF kushambulia kijiji kingine cha karibu cha Kazaramo, ambapo walipambana na jeshi na vikundi vya kujitolea vya raia wa eneo hilo.
ISIS ilitangaza kuhusika na shambulio hilo huko Kazaramo na kusema pia wanachama wake waliwateka nyara na kuwaua watu watatu.