Maporomoko ya udongo mashariki mwa Kongo yauwa takriban watu 13
-
Maporomoko ya udongo Kongo
Takriban watu 13 wamepoteza maisha kufuatia maporomoko ya udongo yaliyotokea mashariki mwa Kongo mapema jana Jumanne. Watu wengien zaidi ya 30 hawajulikani waliko hadi sasa.
Maporomoko hayo yalitokea mwendo wa saa moja asubuhi jana katika kijiji cha Burutsi katika jimbo la Kivu Kaskazini. Walioshuhudia wanasema kuwa maporomoko hayo ya ardhi yalifuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa saa kadhaa na kukata barabara kuu kati ya mji mkubwa wa Goma na makao makuu ya jimbo hilo, Walikale.
Descarte Akilimali mkuu wa eneo la Burutsi ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba kilima kizima kilianguka ndani ya kijiji cha Burutsi wakati watu walipokuwa wamelala.
Maafisa wa eneo la Burutsi katika jimbo la Kivu Kaskazini wameeleza kuwa wameomba msaada wa serikali hata hivyo kufungwa barabara inayoelekea Goma kuimeikwamisha serikali kutoa msaada kwa waathirika.
Mbali na maporpmoko haya ardhi yaliyokiathiri kijiji cha Burutsi katika jimbo la Kivu Kaskakzini, eneo la mashariki kwa Kongo kwa miongo kadhaa sasa limesambaratishwa na machafuko na mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi mbalimbali yenye silaha, ikiwa ni pamoja na waasi wa kundi la M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.
Walikale ambayo ni makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini ulidhibitiwa katika mashambulizi ya waasi wa M23 mwaka jana; na eneo hilo limeendelea kukumbwa na ghasia.
Zaidi ya makundi 100 ya wanamgambo wenye silaha yanapigana katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa Kongo karibu na mpaka na Rwanda.