Rais Kagame ahifadhi kiti chake, ashinda uchaguzi kwa 99%
Matokeo ya awali ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Rwanda (NEC) yanaonyesha kuwa, Rais Paul Kagame yuko kifua mbele kwa kuzoa asilimia 99.15 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika jana Jumatatu.
Mwenyekiti wa NEC, Oda Gasinzigwa amesema Paul Kagame wa chama tawala cha RPF ameiongoza Rwanda kwa kipindi cha miaka 24 sasa, amezoa asilimia 99.15 ya kura 7,160,864 zilizohesabiwa kufikia sasa. Zaidi ya Wanyarwanda milioni tisa wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo wa Rais na Bunge. Wanyarwanda milioni mbili kati yao wanapiga kura kwa mara ya kwanza.
Kwa mujibu wa NEC, wagombea wengine wawili, Frank Habineza wa Democratic Green Party of Rwanda na Philippe Mpayimana, ambaye ni mgombea huru, wamepata chini ya asilimia moja ya kura hizo kila mmoja.
Habineza amepata kura 38,301 sawa na asilimia 0.53 ya kura, huku na Mpayimana akipata kura 22,753 sawa na asilimia 0.32 ya kura. Rais Kagame sasa ataongoza Rwanda kwa muhula wa nne akiwa ameliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwaka 2000; ambapo mwaka 2015 ilifanyika kura ya maoni ambayo iliondoa ukomo wa mihula miwili ya kikatiba kwa marais wa nchi hiyo. Katika uchaguzi uliofuata wa mwaka 2017, Rais Kagame alishinda kwa kuzoa asilimia 98.8% ya kura.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Rwanda amesema ushiriki wa uchaguzi huo wa jana kufikia sasa upo katika kiwango cha asilimia 98. Katika upande wa uchaguzi wa Bunge wagombea 589 wachuana kuwania viti 80 vya Bunge la Rwanda.
Zaidi ya waangalizi 1,100 wa ndani na nje wamesimamia uchaguzi huo. Wakosoaji wanasema wapinzani wakuu wa Rais Paul Kagame kama Diane Rwigara, wamezuiwa kushiriki katika uchaguzi huo.