AU: Afrika ina uhaba wa walimu milioni 15
(last modified Sat, 20 Jul 2024 06:14:25 GMT )
Jul 20, 2024 06:14 UTC
  • AU: Afrika ina uhaba wa walimu milioni 15

Bara la Afrika linakabiliwa na upungufu wa walimu zaidi ya milioni 15. Hayo yamesemwa na Mohammed Belhocine, Kamishna wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Umoja wa Afrika katika kikao na waandishi wa habari pambizoni mwa Kikao cha 45 cha Kawaida cha Halmashauri Kuu ya AU, mjini Accra, Ghana.

Belhocine ameonya kuwa, uhaba huo wa walimu utakuwa na taathira hasi kwa uwezo wa bara Afrika kufikia maazimio yake katika nyuga za elimu na ustawi.

Kamishna huyo wa AU amebainisha kuwa, dola bilioni 90 zinahitajika kuziba pengo hilo ili nchi za Afrika ziweze kuafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kufikia mwaka 2030, kama ilivyoanishwa na Umoja wa Mataifa. 

"Leo hii, ni fakhari kuwa mfanyabiashara kuliko kuwa mwalimu, hili pengo ndilo linalosababisha uhaba mkubwa wa walimu," ameeleza Kamishna wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ubinifu wa Umoja wa Afrika.

Hivi karibuni pia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilieleza katika ripoti yake kwamba, kuna uhaba wa walimu duniani na kuzitaka nchi zote zichukue hatua kukabiliana na suala hilo ambalo taasisi hiyo ya UN imeliita "kadhia ya ulimwengu mzima".

Walimu katika mgomo na maandamano nchini Zimbabwe

UNESCO inasema walimu milioni 44 zaidi wanahitajika ili kufikia lengo la ulimwengu mzima la elimu ya msingi na sekondari ifikapo mwaka 2030, na vilevile walimu wapatao milioni 15 wanahitajika kwa ajili ya eneo la Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara pekee.

Vyama vya walimu vinasema mazingira duni ya kazi, tafrani nyingi na mishahara duni ni miongoni mwa sababu kuu zilizosababisha walimu kuacha kazi katika nchi 79 duniani.