Aug 03, 2024 06:54 UTC
  • Kambi ya upinzani Tunisia yalaani 'mbinyo' wa kabla ya uchaguzi wa rais

Wagombea urais wa kambi ya upinzani nchini Tunisia, mashirika ya kutetea haki za binadamu na vyama vya kisiasa vimelaani 'vizuizi vya kiholela' vilivyowekwa dhidi yao na serikali ya Tunis kabla ya uchaguzi wa Oktoba 6.

Katika taarifa yao, wamesema kwamba vizuizi hivyo vinalenga kuhakikisha Rais Kais Saied anachaguliwa tena.

Viongozi 11 wa upinzani wanatarajia kuchuana na Saied katika kinyang'anyiro cha uchaguzi ujao wa rais. Sheria mpya iliyowekwa na mamlaka husika za Tunisia inawataka wagombea kuwasilisha hati inayothibitisha kwamba hawana rekodi ya uhalifu kabla ya kuwaruhusu kujisajili. Hadi sasa, hakuna hata mmoja wa wagombea wa upinzani aliyepata hati hiyo.

Mnamo 2021, Kais Saied alinyakua madaraka ya nchi na kulivunja Bunge, jambo ambalo lilizusha ukosoaji mkubwa kikanda na kimataifa. 

Baadaye alisimamia uundwaji wa katiba mpya ambayo inampa Rais mamlaka makubwa zaidi na kudhoofisha jukumu la Bunge la kusimamia utendaji wa Serikali.

Vyama vya upinzani nchini Tunisia vilitaja hatua hizo za Rais Kais Saied kuwa ni mapinduzi baridi. 

Tags