Aug 09, 2024 03:27 UTC
  • Watu 26 wahukumiwa kifo Kongo DR kwa 'jinai za kivita'

Watu wasiopungua 26 wamehukumiwa kifo na mahakama ya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya kupatikana na hatia katika mashitaka matatu yaliyokuwa yakiwakabili.

Miongoni mwa waliohukumiwa kifo katika faili hilo ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI), Corneille Nangaa Yobeluo, na wapambe wake.

26 hao walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya 'kula njama dhidi ya dola', jinai za kivita pamoja na kujihusisha na harakati za uasi. Mawakili wa washtakiwa hao wamesema hawakupewa muda wa kutosha wa kujenga hoja za kuwatetea wateja wao.

Kati ya watu hao 26 waliopatikana na hatia, 21 wametoroka nchi, akiwemo Nangaa, ambaye ni kiongozi wa Muungano wa Mto Congo "Alliance Fleuve Congo" (AFC).

Hukumu hiyo imetolewa siku chache baada ya Rais Felix Tshisekedi wa Kongo DR kumtuhumu Rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila kuwa anaunga mkono muungano wa makundi ya waasi yaliyowekewa vikwazo na Marekani.  

Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Uchaguzi ya Kongo (CENI), Corneille Nangaa

Tshisekedi ameeleza kuwa Kabila alisusia uchaguzi na sasa anaandaa uasi kwa sababu yeye ni mwanachama wa AFC. AFC ni harakati ya kisiasa na kijeshi iliyoasisiwa mwezi Disemba mwaka jana nchini Kenya, kwa shabaha ya kuyaunganisha pamoja makundi yanayobeba silaha, vyama vya kisiasa na taasisi za kiraia kabla ya uchaguzi wa rais.

Mapema mwezi uliopita pia, washtakiwa 31, wakiwemo wanajeshi 27 na wake zao wanne ambao ni raia wa kawaida walihukumiwa kifo na mahakama ya kijeshi ya Butembo katika mkoa wa Kivu Kaskazini,  kwa "kutoroka vitani na kumpa nafasi adui".

Aidha mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu wanajeshi wanane wa Kongo walihukumiwa kifo huko Goma kwa "uoga" na "kuwakimbia adui".

Tags