Aug 10, 2024 11:14 UTC
  • Ujangili wa Magharibi umepunguza mno idadi ya simba barani Afrika

Huku ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Simba Duniani leo Agosti 10, imebainika kuwa idadi ya mnyamapori huyo inapungua kwa kiwango cha kutisha barani Afrika kutokana na ujangili unaofanywa na nchi za Magharibi.

Shirika la habari la Anadolu limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, simba waliochukuliwa kutoka katika makazi yao ya mwituni barani Afrika na kulelewa wakiwa 'mateka' wanachinjwa kwa ajili ya kufurahisha watalii, hasa kutoka nchi za Magharibi, huku Marekani ikiwa mchangiaji mkubwa.

Simba wa mwituni, ambao wamepoteza idadi kubwa ya wakazi na makazi yao kutokana na 'shughuli za binadamu' katika karne iliyopita, wanatatizika kuishi katika misitu (savanna) inayotoweka ya Afrika.

Kulikuwa na simba wapatao 200,000 porini mwanzoni mwa karne iliyopita, kulingana na makadirio ya Kitengo cha Utafiti wa Uhifadhi wa Wanyamapori cha Chuo Kikuu cha Oxford. Kufikia mwisho wa karne iliyopita, idadi ambayo ilikuwa imepungua hadi karibu 33,000 kutokana na uwindaji na mambo mengine ya kibinadamu, ilipungua kwa 43% tangu mwaka 2001.

Mbuga ya Kyambura nchini Uganda

Leo hii, inakadiriwa kuwa simba 23,000 pekee ndio wamesalia maporini. Wakiwa wamepoteza karibu 95% ya makazi yao ya asili ya kihistoria, simba leo hii kimsingi wanaishi katika mbuga za kitaifa zinazolindwa vyema kama katika nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Botswana, Namibia, Zambia na Zimbabwe.

Afrika Kusini, ambayo ni mwenyeji wa mojawapo ya idadi kubwa zaidi ya simba duniani, ina takriban 3,500. Si vibaya kuashiria hapa kuwa, bara la Afrika lilikuwa na ndovu milioni 13 mwaka 1979, lakini kushadidi ujangili na magendo ya vipusa kumesababisha idadi hiyo kupungua hadi laki 4 hivi.

Tags