Tanzania yatakiwa kuheshimu haki za binadamu kuelekea uchaguzi serikali za mitaa
(last modified Thu, 17 Oct 2024 11:15:53 GMT )
Oct 17, 2024 11:15 UTC
  • Tanzania yatakiwa kuheshimu haki za binadamu kuelekea uchaguzi serikali za mitaa

Shirika la kimatatifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Tanzania kulinda haki za binadamu kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.

Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi wa serikali za mtaa tarehe 27 Novemba  mwaka huu huku wapiga kura wakitarajiwa kuchagua Mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi mchanganyiko la wanaume na wanawake), wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi la wanawake) na wenyeviti wa vitongoji katika Mamlaka za Wilaya.

Nafasi zingine zinazotarajiwa kugombaniwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo, Mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake) na wajumbe wa kamati ya mtaa (Kundi la Wanawake) katika Mamlaka za Miji.

Hata hivyo, Human Rights Watch inadai kuwa, ndani ya miezi michache iliyopita kumekuwepo na matukio mengi ya uvunjifu wa haki za binaadamu nchini Tanzania hali inayotia hofu kuelekea uchaguzi huo.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania

 

“Tangu mwezi Juni, mamlaka zimewakamata kiholela mamia ya wafuasi wa upinzani, zimedhibiti upatikanaji wa mitandao ya kijamii, zimefungia vyombo huru vya habari, na zimehusishwa na kutekwa na mauaji ya wapinzani wa serikali wasiopungua wanane” imesema sehemu ya ripoti ya Human Rights Watch.

Hatahivyo akizungumza, waziri wa sheria na katiba nchini humo Palamagamba Kabudi amesema madai hayo yamejazwa chumvi na kwamba hayaendani na hali halisi nchini Tanzania.

Bwana Kabudi ameitetea serikali ya Tanzania akisema kwamba imekuwa kifua mbele kulinda haki za kibinadamu na kwamba uchaguzi wa mitaa utakaofanyika mwezi ujao utakuwa huru na wa haki.