Araghchi: Iran haitafanya mazungumzo chini ya mashinikizo
Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Tehran iko tayari kuketi katika meza ya mazungumzo ya nyuklia na Troika ya Umoja wa Ulaya kulingana na maslahi na haki za Iran na si chini ya mashinikizo na vitisho.
Araqchi ameeleza haya katika ujumbe aliotuma katika mtandao wa X baada ya mazungumzo muhimu na ya wazi jana mjini Tehran na Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
"Mpira upo katika uwanja wa Umoja wa Ulaya na nchi tatu za Troika ya umoja huo. Tufanya mazungumzo kulingana na maslahi ya taifa na haki za Iran zisizoepukika', amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.
Araqchi ambaye alikuwa miongoni mwa wapatanishi wakuu katika mazungumzo ya nyuklia kati ya Tehran na madola makuu ya dunia yaliyopelekea kufikiwa makubaliano ya nyuklia mwaka 2015 kwa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) amesisitiza kuwa Iran ambayo ni mwanachama mwajibikaji wa Mkataba wa NPT itaendeleza ushirikiano wake kamili na wakala wa IAEA.
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA aliwasili Tehran juzi Jumatano usiku akiongoza ujumbe wa wakala huo kwa lengo la kuzungumza na viongozi wakuu wa masuala ya nyuklia na kisiasa wa Iran.
Ziara ya juzi ya Grossi ni muendelezo wa majadiliano kati ya Iran na wakala wa IAEA.