Kiongozi mmoja wa HAMAS auawa katika jela za Israel
Mmmoja wa viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, Samih Aliwi, aliuawa shahidi jana Ijumaa, Novemba 15, 2024 ikiwa ni siku sita baada ya kuhamishwa kutoka gereza la Ramla na kupelekwa katika hospitali ya Assaf Harofeh. Taarifa nyingine zinasema aliuawa shahidi tangu siku sita nyuma lakini utawala wa Kizayuni ulikuwa unaficha kifo chake.
Kamanda Samih Aliwi mwenye umri wa miaka 61 ni kutoka kambi ya wakimbizi ya Nablus ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kabla ya kupelekwa kwenye Gereza ya Ramla, kiongozi huyo wa HAMAS alikuwa anashikiliwa kinyume cha sheria katika gereza jingine la kuogofya la Negev.
Aliwi, aliyekuwa anazuiliwa kwenye mikono katili ya utawala wa Kizayuni tangu Oktoba 21, 2023, alikuwa na matatizo ya afya ikiwa ni pamoja na uvimbe mbaya wa utumbo lakini utawala wa Kizayuni ulikataa kumpa matibabu na uliendelea kumuweka sehemu nzito sana ambazo haziendani na hali yake ya kiafya mpaka ameuawa shahidi.
Kiongozi mwingine wa HAMAS anayejulikana kwa jina la Anwar Aslim kutoka Ukanda wa Ghaza aliuawa shahidi Alkhamisi wakati alipokuwa anapelekwa hospitalini kutoka jela ya kutisha ya Negev.
Kwa kuuawa wanamapambano hao wawili kunaifanya idadi ya mateka wa Palestina waliouawa shahidi hadi hivi sasa katika jela za kutisha za Israel tangu tarehe 7 Oktoba 2023 kufikia mateka 43. Idadi hiyo imechujwa kupindukia na utawala wa Kizayuni kwani kuna mamia ya Wapalestina wanaotekwa nyara na halafu taarifa zao zinapoteza kikamilifu.