Jeshi la Congo DR limekomboa mji wa Kalembe, Kivu Kaskazini
(last modified Wed, 23 Oct 2024 07:57:59 GMT )
Oct 23, 2024 07:57 UTC
  • Jeshi la Congo DR limekomboa mji wa Kalembe, Kivu Kaskazini

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) limetangaza kuwa limefanikiwa kukomboa mji wa Kalembe ulioko katika mkoa wa Kivu Kaskazini kutoka kwa waasi wa M23.

Msemaji wa jeshi la Congo DR, Sylvain Ekenge, amesema maofisa wake wamefanikiwa kukomboa Kalembe, na kwamba mapigano makali yanayoendelea katika maeneo ambayo hayajadhibitiwa na jeshi la serikali.

Hata hivyo waasi wa M23 wamekanusha habari hiyo wakisema bado wanalidhibiti eneo hilo la Kalembe.

Kalembe iko katika jimbo la Kivu Kaskazini, ambalo limeathirika sana tangu kundi la M23 lianzishe uasi upya mashariki mwa nchi hiyo, miaka 2 iliyopita.

Congo na Umoja wa Mataifa zinaituhumu nchi jirani ya Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi hilo la waasi, madai ambayo yanakanushwa vikali na sereikali ya Kigali.

Mamilioni ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo, ambayo pia yamezidisha mgogoro wa binadamu huko Kivu Kaskazini.