Ramaphosa: Daima tutaendelea kuwa pamoja na taifa la Palestina
(last modified Thu, 24 Oct 2024 11:52:56 GMT )
Oct 24, 2024 11:52 UTC
  • Ramaphosa: Daima tutaendelea kuwa pamoja na taifa la Palestina

"Afrika Kusini na Palestina daima zitakuwa pamoja," hiyo ni ahadi iliyotolewa na Rais Cyril Ramaphosa wakati alipoonana na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Palestina Mahmoud Abbas walipokutana ana kwa ana pembeni mwa mkutano wa kilele wa BRICS katika mji wa Kazan nchini Russia.

Afrika Kusini ni mwanachama mwanzilishi wa BRICS ambalo ni kundi la nchi zinazozidi kustawi kiuchumi huku Palestina ikiwa mwalikwa wa mkutano huo wa 16 wa wakuu wa mataifa ya BRICS.

Viongozi hao wawili wamejadiliana fursa za kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kwa kuzingatia maslahi yao ya kitaifa, ya kieneo na ya kimataifa. 

Afrika Kusini ilifungua kesi katika mahakama ya ICJ iliyoko The Hague Uholanzi mwishoni mwa 2023, ikiishutumu Israel kutokana na jinai zake kubwa huko Ghaza Palestina.

Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Uturuki, Nicaragua, Palestina, Uhispania, Mexico, Libya na Colombia zimejiunga na kesi hiyo ambayo ilianza kusikilizwa hadharani mwezi Januari mwaka huu.

Mwezi Mei, Mahakama ya ICJ iliiamuru Israel kusitisha mashambulizi yake katika mji wa wa Rafah wa kusini wa Ghaza. Hiyo ilikuwa ni mara ya tatu kwa jopo la majaji 15 kutoa maagizo ya kutaka kudhibitiwa utawala wa Kizayuni. 

Hapo awali, wakati akihutubia mkutano wa kilele wa BRICS, Ramaphosa alisema nchi za dunia zina jukumu la kutofadhili mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.

Rais Ramaphosa vile vile amesema, wakati dunia inashuhudia hali mbaya inayoendelea ya watu wa Palestina, Afrika Kusini inalazimika kuunga mkono roho ya mshikamano wa kuwatetea Wapalestina.