Upinzani DRC wauonya utawala kuhusu mageuzi ya katiba
Martin Fayulu mmoja wa viongozi wa upinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amewaambia waandishi wa habari kwamba hakutakuwa na mageuzi au mabadiliko yoyote ya Katiba kabla ya uchaguzi mkuu wa 2028.
Martin Fayulu, ambaye alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa mwaka jana, amesema Katiba ya sasa haimzuii mtu yeyote kufanya kazi. Kiongozi huyo wa upinzani ametoa wito kwa raia wa Kongo kuwa tayari kuzuia jaribio lolote la magaeuzi ya katiba.
Akiwa ziarani mjini Kisangani, Kaskazini-Mashariki mwa Kongo, Rais Felix Tshisekedi aliahidi kuteua mwakani, tume ya kitaifa kwa ajili ya kuandaa katiba mpya.
Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, idadi ya mihula ya urais haitabadilishwa, lakini wapinzani wake wanasema ana nia ya kuwania muhula wa tatu.
Pamoja na hayo Rais Félix Tshisekedi, anasema kuwa katiba ya nchi hiyo inapaswa kurekebishwa kwa sababu ina "udhaifu" fulani.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Tshisekedi kuzungumza hadharani kuhusu suala hilo lenye utata, baada ya chama chake cha UDPS kuanzisha kampeni mwezi huu ya kufanyia marekebisho katiba.
Hayo yanajiri katika halii ambayo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa usalama mashariki mwa nchin hiyo.
Wimbi la mashambulizi mapya ya waasi wa M23 na ADF linaendelea kuwatesa wananchi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku mapigano baina ya wanajeshi wa serikali na waasi wa makundi hayo mawili yakiendelea.