Watoto milioni 3.7 wako katika hatari ya utapiamlo mkali nchini Sudan
Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yamesema kuwa, watoto milioni 3.7 walio na umri wa chini ya miaka mitano nchini Sudan wako katika hatari ya kukabiliwa na utapiamlo na kuonya kuhusu hali mbaya zaidi ya kibinadamu kote nchini humo.
Shirika la Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) yametoa taarifa hiyo ya pamoja na kusema: "Kuna watoto milioni 3.7 walio na umri wa chini ya miaka mitano wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali mwaka huu pekee na wanahitaji matibabu ya dharura ya kuokoa maisha yao."
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watoto hao tayari wamedhoofishwa na njaa. Ikiwa misaada haitawafikia haraka, kuna uwezekano wa mara 11 wa kufariki dunia watoto hao kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Maafisa wawili wakuu, yaani Kamishna Mkuu Msaidizi wa Operesheni wa UNHCR, Raouf Mazou, na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Ted Chaiban, vile vile wamesisitiza kuwa, suala muhimu katika utoaji wa misaada ni kuhakikisha jamii zinazohitaji msaada kote nchini Sudan zinafikiwa kwa usalama na bila ya vizuizi vyovyote.
Wamesema, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na utoaji wa misaada yanahitaji kuruhusiwa na mamlaka zinazodhibiti maeneo mbalimbali kuzifikia jamii zilizoathirika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sudan hivi sasa ni moja ya sehemu zenye majanga kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, ambapo zaidi ya watu milioni 11 wamekimbia makazi yao, ndani na nje ya mipaka ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nusu ya wakazi wa Sudan yaani takriban watu milioni 25 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi nchini humo.